Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

TANZANIA NA KENYA ZAAMUA KUIIMARISHA BIASHARA, KUONDOA VIKWAZO


Katibu Mkuu wa Biashara katika Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda wa Kenya, Bi. Regina Ambam amesema kuwa Kenya na Tanzania zimeamua kuimarisha mustakabali wa biashara baina yao, bara la Afrika na hata katika mazingira ya Biashara ya kimataifa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Oktoba 1, 2025, katika mkutano wa kuondoa vikwazo vya kibiashara kati ya nchi hizo mbili, Bi. Ambam alisema hatua hiyo inalenga kuondoa changamoto zinazokwamisha ufanisi wa biashara na kuhakikisha kuwa Wananchi wananufaika moja kwa moja na ushirikiano huo.

Alifafanua kuwa mkutano huo umetazama kwa undani vikwazo vilivyokuwa vikileta ugumu katika kufanya biashara kwa ufanisi kati ya Tanzania na Kenya. Aliongeza kuwa wamejiridhisha kwamba biashara kati ya nchi hizo mbili ni ya uhakika, yenye ufanisi na inayowanufaisha wananchi, na kwamba ni lazima kuhakikisha vizuizi vyote vinavyokwamisha biashara vinaondolewa.

Aidha, Bi. Ambam alibainisha kuwa maamuzi yaliyofikiwa yameweka mazingira rafiki zaidi ya biashara baina ya mataifa hayo mawili. Alisema hatua hiyo si muhimu tu kwa Tanzania na Kenya pekee, bali pia kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla.

Alisisitiza kuwa kwa kuboresha mazingira ya biashara kati ya Kenya na Tanzania, mfumo mzima wa biashara wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unalindwa kwa kuwa mtikisiko wowote katika moja ya nchi hizi mbili huathiri wanachama wengine. Kwa mujibu wake, ushirikiano huu unaimarisha biashara, unarahisisha ufanisi, unawawezesha Wananchi kufanya biashara kwa amani na tija, na ni ishara ya ustawi unaokuja katika ukanda wa Afrika Mashariki.