Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

TANZANIA KUNA UHURU WA KUTOSHA WA KUFANYA BIASHARA NA UWEKEZAJI: PROF. MKUMBO


Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo amewahakikishia wawekezaji na wafanyabiashara kuwa Tanzania kuna uhuru wa kutosha wa kufanya biashara na uwekezaji hivyo Serikali itaendelea kutekeleza wajibu wake kikamilifu ikiwemo kuweka mazingira mazuri ya sera na  sheria ili wafanye biashara katika utulivu na  kupata faida hatimaye Serikali iweze kufaidika kupitia ajira kwa wananchi na kupata kodi.

 

Prof. Mkumbo ameyasema hayo Novemba 23, 2021 Dar es salaam alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kuadhimisha miaka 60 ya kuanzishwa kwa kiwanda cha Sigara (TCC)

 

“Tunatambua kwamba  ili uchumi wetu uendelee kukua na kufikia malengo tuliyojiwekea katika mpango wa tatu wa maendeleo wa miaka mitano 2021/22 – 2025/ 26 tunahitaji uwekezaji uliopo nchini uendelee kufanya kazi vizuri kwa utulivu lakini pia tupate uwekezaji mpya” amessema Prof. Kitila Mkumbo

 

Prof. Mkumbo ameeleza kuwa Tanzania kuna utulivu wa siasa na amani ya kutosha ambacho ndicho kigezo cha kwanza kwa wawekezaji wote duniani na  Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu mbalimbali ya kuwezesha uzalishaji  viwandani kama barabarabara na maji ikiwemo kufanyia kazi na kumaliza changamoto ya umeme kupitia miradi mbalimbali inayokutekelezwa hapa nchini.

 

Prof. Mkumbo ametoa wito kwa wenye viwanda na wawekezaji kuhakikisha wanazingatia kikamilifu sheria na kanuni zinazoongoza sekta ya viwanda hapa nchini ikiwemo kuheshimu sheria zinazohusu kazi ili watumishi wanaoajiri wafanye kazi katika mazingira mazuri na walipwe ujira sitahiki kwa mujibu wa sheria.

 

Aidha, Prof. Mkumbo ametoa rai kwa makampuni na wafanyabiashara wa Tanzania kujikita katika ushindani katika kipindi hiki ambacho Tanzania imejiunga katika mkataba wa eneo huru la biashara (AfCFTA) wenye nchi wanachama 54.

 

Kwa upande wake, Naibu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Patrobas Katambi amepongeza kampuni ya TCC kwa kuweza kutoa ajira za moja kwa moja Zaidi ya 418 na ajira nyinginye zisizo za kudumu vilevile amepongeza kampuni kwa kuendelea kutoa fedha kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii itakayowasaidia wafanyakazi watakapomaliza kazi wapate pesa za kuwasaidia katika kipindi ambacho hawapo kazini.

 

Nae, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya TCC, Michal Bachan amesema kuwa wanajivunia kwa kipindi cha miaka 60 ya kuanzishwa kwao, kampuni ya TCC imekuwa na safari yenye mafanikio ambayo imesaidia kampuni hiyo kuwa na mchango mkubwa katika pato ya Serikali ambayo imeongezeka kufika wastani wa bilioni 220.