Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

TANZANIA KUJENGA UCHUMI WA UZALISHAJI NA USHINDANI WA KIMATAIFA


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka mkakati wa kimkakati wa kuachana na uchumi unaotegemea rasilimali asilia na kuelekea katika uchumi unaojengwa juu ya uzalishaji, uongezaji thamani na ushindani wa kimataifa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufikia lengo la kuwa nchi yenye pato la dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.


Hayo yamebainishwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb) wakati wa ziara yake katika Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC), Disemba 22, 2025 jijini Dar es Salaam.
Mhe. Kapinga ameongeza kuwa mwelekeo huo ni msingi wa mageuzi ya kiuchumi yanayolenga kukuza viwanda, kuongeza thamani ya mazao ya ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Aidha, amesisitiza kuwa kufanikisha dira hiyo, hakuna budi kuwepo ushirikiano wa karibu na endelevu kati ya Serikali na sekta binafsi, hususan katika kuimarisha uzalishaji wa ndani, kuvutia uwekezaji, na kujenga mazingira rafiki ya biashara yanayochochea ushindani wa kimataifa.

Kwa upande wake, rais wa Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC), Bw. Vicent Minja, amesema chemba hiyo imeendelea kuwa nguzo muhimu kwa wafanyabiashara nchini, hasa kutokana na mageuzi ya kimfumo na kimkakati inayoyatekeleza ili kuhakikisha sekta binafsi inashirikiana kikamilifu na Serikali katika kutekeleza malengo ya kitaifa ya maendeleo.

Bw. Minja ameongeza kuwa TNCC inaendelea kuimarisha nafasi yake kama jukwaa la kutatua changamoto za wafanyabiashara, kuchochea ukuaji wa Viwanda na kushiriki katika ajenda ya kitaifa ya kutengeneza ajira endelevu.

Hatahivyo baadhi ya wawakilishi wa TNCC kutoka mikoa mbalimbali, wameishukuru Serikali kwa kuendelea kujenga mazingira wezeshi ya Biashara nchini. Wamewahimiza wafanyabiashara kujiunga na Chemba ya Taifa ya Biashara ili kupata jukwaa la pamoja la kufikisha changamoto zao kwa urahisi na kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo ya kiuchumi.

Ziara hiyo omekuwa nguzo imara ya kuimarisha kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika safari ya kuijenga Tanzania yenye uchumi imara, shindani na jumuishi ifikapo mwaka 2050.