Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

TBS na CAMARTEC zatakiwa kuongeza wigo wa huduma


TBS na CAMARTEC zatakiwa kuongeza wigo wa huduma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeliagiza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kupanua wigo wa utoaji huduma katika kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinakuwa na viwango na ubora unaohitajika katika soko.

Vilevile, imekiagiza Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) kupanua wigo wa utengenezaji zana za kilimo zenye ubora na kwa bei nafuu ambayo wakulima wa chini wanaweza kuzimudu.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Deodatus Mwanyika ( Mb) wakati wa uwasilishaji wa Taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TBS na CAMARTEC zilizochini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Kamati hiyo Oktoba 24, 2024 katika ukumbi wa Bunge, Jijini Dodoma.

Aidha, Wajumbe wa Kamati hiyo walipata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali yaliyolenga kuboresha utendaji kazi wa TBS na CAMARTEC ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wakubwa kupata huduma, kurasmisha bidhaa zao, kupata nembo za ubora na bidhaa kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

Naye, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe. Balozi Dkt. John Stephen Simbachawene, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara Bw. Needpeace Wambuya na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Biashara Bw. Sempeho Manongi ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara yake itayafanyia kazi maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa na kuahidi kushirikiana na Kamati hiyo katika kuiwezesha TBS na CAMARTEC kutejeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Akitoa maelezo kwa Kamati hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania Dkt. Ashura Katunzi amesema TBS inajukumu la kukuza viwango, usalama na uhakiki wa ubora katika viwanda na biashara kupitia uandaaji wa viwango, uhakiki wa ubora, usajili, ukaguzi, upimaji na huduma za ugezi kwa maendeleo endelevu ya kijamii na uchumi.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa CAMARTEC Mhandisi. Godfrey Mwinama akitoa maelezo kwa Kamati hiyo, amesema CAMARTEC inajukumu la kuendeleza mbinu za kilimo na teknolojia vijijini kupitia utafiti na maendeleo kwa maendeleo endelevu.