Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Tume ya Ushindani (FCC) imefanya semina kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC)


Tume ya Ushindani (FCC) imefanya semina kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) iliyofanyika katika ukumbi wa PSSSF uliopo Makole Jijini Dodoma. 

Kamati hiyo imepokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya Ushindani (FCC) ambayo ipo chini ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ambapo awali akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu hayo, Bw. William Erio, Mkurugenzi Mkuu wa FCC amebainisha kuwa Taasisi hiyo iliyoanzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 62 (1) cha Sheria ya Ushindani Na. 8 ya Mwaka 2003, kwa madhumuni ya kukuza na kulinda ushindani katika biashara na kumlinda mtumiaji dhidi ya mienendo hadaifu na kandamizi katika uchumi wa soko.

Bw. Erio ameongeza kuwa, FCC pia ina jukumu la kudhibiti biashara ya bidhaa bandia kwa mujibu wa Sheria ya Alama za Bidhaa Na. 20 ya Mwaka 1963 na marekebisho yake.

"Lengo kuu la Sheria ya Ushindani ni kuongeza ufanisi katika uzalishaji, usambazaji na ugavi wa bidhaa na huduma katika kuhakikisha mazingira sawa ya ukuaji wa uchumi baada ya Taifa kuondokana na mfumo wa uchumi hodhi na kuhamia katika mfumo wa uchumi wa soko huria kwa maslahi mapana ya Taifa", amesema Bw. Erio. 

Naye Mhe. George Malima ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), amesema kuwa amefurahishwa na utendaji kazi wa Tume ya Ushindani (FCC) na amewaasa waendelee kuhakikisha wanadhibiti bidhaa bandia kwa lengo la kumlinda mtumiaji wa mwisho.

Aidha, Waheshimiwa wajumbe wa Kamati hiyo wametoa michango mbalimbali ikiwa ni pamoja na  FCC kusaidiwa kuongeza idadi ya watumishi ili kukidhi mahitaji katika kutekeleza majukumu yake kama vile udhibiti wa bidhaa bandia katika mipaka yote ya nchi na njia zote zisizo rasmi zinazotumika kupitisha au kuingiza bidhaa hizo, kutoa elimu kwa wabunifu, watengenezaji wa bidhaa na watumiaji wa bidhaa mbalimbali ili wawe na uelewa wa bidhaa bandia na bidhaa halisi, kuwajengea uwezo na utaalam ikiwa ni pamoja na kuwapatia vifaa vya kuteketeza bidhaa bandia bila kuathiri mazingira, kuwapa nguvu ya usimamizi na utekelezaji wa Sheria wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Aidha Waheshimiwa wajumbe wa kamati hiyo wamesema kuwa kuna haja kubwa FCC ikaongezewa bajeti kulingana na majukumu wanayofanya ukizingatia nchi yetu sasa imeshajiunga katika masoko mbalimbali yakiwemo EAC, SADC na AfcFTA ambapo uingizwaji wa bidhaa bandia kupitia njia zisizo rasmi utakuwa mkubwa. 

Akijibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na Wajumbe wa Kamati, Dkt. Aggrey Mlimuka, Mwenyekiti wa Bodi ya FCC ameeleza njia zinazotumika kupambana na bidhaa bandia kama vile kutoa elimu kwa wafanyabiashara na watumiaji kupitia jumuiya zao kuhusiana na matakwa ya Sheria ya Alama za bidhaa ya Mwaka 1963 na marekebisho yake. 

Dkt. Mlimuka ameongeza kuwa bidhaa bandia zina madhara makubwa katika uchumi wetu, ikiwa ni pamoja na ukwepaji kodi, kutowajibika wakati wa athari, kuibiwa au kudanganywa bei pamoja na kukithiri kwa bidhaa duni sokoni.
"FCC tumekuwa tukitekeleza majukumu yetu kwa mujibu wa Sheria, ufanisi na mafanikio makubwa tangu wakati wa Serikali ya awamu ya tatu tulipoingia katika utaratibu wa soko huria, ni dhahiri wakati wote huo FCC imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa weledi, kuepusha athari zinazoweza kumuathiri mtumiaji na hivyo kuifanyia Taasisi hii kuwa na mchango mkubwa na wenye tija katika ukuaji wa uchumi katika Taifa letu"