Habari
Uhusiano wa Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu umekua kwa kiasi kikubwa kwenye mauzo ya ndani na nje.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo (Mb) amesema Uhusiano wa Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu umekua kwa kiasi kikubwa kwenye mauzo ya ndani na nje.
Amebainisha hayo Desemba 02,2024 Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Miaka 53 ya Taifa hilo la Falme za Kiarabu (UAE).
Amesema Umoja huo wa UAE ni mojawapo ya washirika wakuu wa biashara Tanzania na Afrika Mashariki kwani katika miaka ya hivi karibuni, kiwango cha biashara kati ya mataifa hayo mawili kimeongezeka kwa kiasi kikubwa, ambapo mauzo ya nje kutoka Tanzania kwenda UAE yalikuwa na thamani ya dola bilioni 1.07 mwaka 2022, ikiwemo bidhaa za kilimo, madini na nguo, huku UAE inauza Tanzania kwa thamani ya dola bilioni 2.48, ikiwa ni pamoja na Petroli, mashine, vifaa vya umeme na ujenzi.
Dkt. Jafo amesema Uhusiano huo wa kibiashara ni uthibitisho wa kuimarika kwa uhusiano baina ya nchi hizo mbili na kuongezeka kwa maslahi kutoka kwa UAE katika masoko mbalimbali Tanzania.
Aidha amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira wezeshi kwa Wawekezaji na Wafanyabiashara hao ili kukuza uwekezaji Nchini.
Nae Balozi wa Falme za Kiarabu Mhe.Khalifa Abdulrahman Al Marzouq amesema Serikali hizo zitaendelea kushirikiana katika Diplomasia,Uwekezaji na Biashara ili kuunganisha Mataifa hayo zaidi.