Habari
Wadau wa Sekta Binafsi wajadili Mwelekeo wa Sera ya Maendeleo ya Viwanda vidogo na Biashara ndogo

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abadallah amewataka wadau wa warsha ya kujadili Mwelekeo wa Sera ya Maendeleo ya Viwanda vidogo na Biashara ndogo kutoa mapendekezo yatakayoiboresha zaidi ili kupata sera inayokidhi mahitaji na hasa katika dunia ya leo.
Naibu Katibu Mkuu aliyasema hayo, alipokuwa akifungua warsha ya wadau kujadili ‘Mwelekeo wa Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo’ nchini uliofanyika Juni 17, 2021 jijini Dar es salaam.
Dkt. Abdallah amewataka wajumbe waliopata fursa hiyo kuhakikisha wanatoa maoni bila kujipendelea wao pekee, bali kwa kuzingatia maslahi ya wajasiliamali wote kwa kuwa sekta hiyo inatoa ajira kwa zaidi ya Watanzania milioni nane.
Aidha, aliwataka washiriki hao kutambua kuwa Sera ya Maendeleo ya Viwanda vidogo na Biashara ndogo nchini inayoandaliwa inabeba wajasiriamali zaidi ya milioni 4.5, hivyo inahitaji umakini katika maandalizi yake ili kuja na suluhisho ya changamoto nyingi kwa wajasiliamali.
Dkt. Abdallah alibainisha kuwa Serikali inatambua na kuthamini umuhimu wa sekta binafsi nchini hususan thamani ya uendelezaji wajasiriamali katika kuendeleza shughuli za uchumi wa nchi.
“Kwa bahati nzuri zaidi, sekta hii ndio inayobeba takribani asilimia 98 ya viwanda vyote nchini. Hii ni faraja kwa kuwa malighafi za nchi yetu hasa za wakulima zinapata masoko katika viwanda hivyo hasa ikizingatiwa viwanda vya sekta hii vimesambaa nchini kote na vingi vikijihusisha katika uongezaji thamani hasa wa mazao ya kilimo,” alisema
Pia Dkt Abdallah alisema Dira ya Taifa 2025, Ilani ya CCM ya 2020 -2025 na Mpango wa Tatu wa Miaka Mitano wa Maendeleo, pamoja na mambo mengine zinatilia mkazo kuishirikisha ipasavyo sekta binafsi katika kuendeleza au kukuza ujasiriamali katika biashara zinazochochea mauzo ya nje ili kuleta uwiano wa maendeleo.
Naye, Mkurugenzi wa Mfuko wa Kuendeleza Huduma za Fedha (FSDT), Irene Mlola, alisema takwimu zinaonesha kuwa, viwanda vidogo na biashara ndogo nchini Tanzania inachangia asilimia 35 ya pato la taifa.
Bi Mlola aliongeza kuwa kumekuwa na ongezeko la wajasiriamali kutoka milioni 15 mwaka 2002 ilipoanzishwa sera iliyopo hadi milioni 4.5 mwaka 2019 ambayo ni matokeo ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo ya Mwaka 2003.
Naye, Mratibu wa Mabaraza ya Kukuza Ujuzi ya Kisekta katika Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Jane Gonsalves, alisema wadau wa sekta binafsi wanaisubiri kwa hamu sera hiyo huku wakitambua ukweli kuwa, sekta binafsi ndio injini ya uchumi wa taifa.
“Bila sekta hii, hatuwezi kupatata maendeleo na tunashukuru juhudi za Wizara katika kufanikisha upatikanaji wake ili iwe yenye msaada na manufaa kwa wafanyabaishara ndogo, wenye viwanda vidogo na Watanzania kwa jumla,” alisema Bi Gonsalves.