Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Exaud Kigahe(Mb) amewapongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa juhudi za kufanya maboresho ya huduma za Sajili na Leseni kwa njia ya mtandao kupitia mifumo ya Usajili kwa njia ya Mtandao (Online Registration System) na Dirisha la Taifa la Biashara (Tanzania National Business Portal).
Amebainisha hayo katika Mkutano wa BRELA na Wadau wake, Oktoba 25,2024 Jijini Dar es Salaam wenye lengo la kujadili fursa na mafanikio, pamoja na changamoto zilizopo na namna Taasisi hii ilivyojipanga kwa ajili ya kuwahudumia wadau wake siku za Mbeleni.
Naibu Waziri Kigahe amesema Mifumo hiyo imepunguza muda, gharama na bughudha kwa Wawekezaji na Wafanyabiashara ambao walikuwa wanasafiri umbali mrefu kufika katika Ofisi za BRELA Dar es Salaam kwa ajili ya kupata huduma hizo.
Mhe.Kigahe pia amesema amevutiwa na Kauli Mbiu ya Mkutano huo inayosema “Mifumo ya Kitaasisi inayosomana na Uwezeshaji wa Biashara nchini” kwani ina akisi maelekezo ya Serikali ya kwamba ifikapo Mwezi Desemba, 2024 Taasisi kuwa na mifumo inayosoamana.
Aidha ametoa rai kwa Taasisi zingine za Serikali ambazo hazina utaratibu wa kuwakutanisha wadau wake kuweza kuiga mfano huo mzuri ili kuweza kujipima kwa kupata maoni na mtazamo kutoka kwa wadau badala ya kujifungia na kujitathmini wenyewe maofisini.
Vilevile amesema Serikali imejipambanua kwa uwazi kabisa kwa dhamira ya kuboresha mazingira ya Biashara na Uwekezaji kwa kuziwezesha Taasisi za Serikali kwa kutoa miongozo, kuzipa rasilimali fedha, rasilimali watu na vitendea kazi ili watimize wajibu wao kwa ufanisi mkubwa na kufikia malengo ya Serikali.
Kwa Upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Ndg.Godfrey Nyaisa amesema Mkutano huo wa Pili wa BRELA na wadau wake una washiriki kutoka Sekta za Umma kwa maana ya Wizara mbalimbali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekta Binafsi zenye mashirikisho yenye wanachama wengi, Wawekezaji, Wamiliki wa Viwanda, Wafanyabiashara, Wajasiriamali, Wabunifu, Ofisi za Mawakili na wafanyabiashara wadogo kabisa hivyo Mchanganyiko huo utaleta majadiliano yenye tija kwa manufaa ya pande zote mbili.