Habari
Wanasayansi wa chakula wana jukumu kubwa katika kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata chakula
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt.Suleiman Serera amesisitiza kuwa wanasayansi wa chakula wana jukumu kubwa katika kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata chakula chenye ubora na usalama unaostahili.
Amebainisha hayo wakati akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo katika mkutano Mkuu wa Chama cha Wanasayansi na Wataalamu wa Teknolojia ya Chakula Tanzania (TAFST) uliofanyika Jijini Dar es Salaam Februari 01,2025.
Dkt.Serera amesema kuwa serikali inatambua changamoto zinazoikabili sekta ya chakula, ikiwa ni pamoja na upotevu wa mazao baada ya mavuno, masuala ya usalama wa chakula, na upungufu wa ongezeko la thamani ambapo ameongeza kuwa sayansi ya chakula na teknolojia zinaweza kusaidia kutatua changamoto hizo.
Aidha amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wanasayansi wa chakula na wataalamu wa teknolojia ya chakula ili waweze kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya taifa ambapo amesema Baadhi ya hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kuimarisha Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kusaidia wajasiriamali wadogo na wa kati, kuongeza uwekezaji katika miundombinu, na kushirikiana na mashirika ya kimataifa.
Dkt.Serera ameongeza kuwa Mkutano huo pia ni muhimu kwa mustakabali wa sekta ya chakula nchini, na unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata chakula bora na salama kwa wote.