Habari
Warsha ya 28 ya Repoa yalenga kuoanua biashara na ukuaji endelevu
Warsha ya 28 ya Repoa yalenga kuoanua biashara na ukuaji endelevu
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe. Balozi Dkt. John Stephen Simbachawene amesema Warsha ya 28 ya Utafiti ya Mwaka ya REPOA (ARW) 2024 inatoa fursa ya kujenga ushirikiano
katika kuongeza uzalishaji, upanuzi wa biashara, huduma za fedha
na ukuaji endelevu kwa ajili ya mustakabali wa Nchi za Afrika kusini mwa Sahara.
Ameyasema hayo Oktoba 25, 2024 jijini Arusha alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu Warsha hiyo inayotarajiwa kufanyika Oktoba 29 - 30, 2024 ikiongozwa na kauli mbiu isemayo "Utafutaji wa ukuaji endelevu na upanuzi wa biashara”
Aidha, Balozi Simbachawene amebainisha kuwa Warsha hiyo inalenga kutafuta moja ya kipaumbele cha msingi cha Tanzania na Nchi Washirika katika kujikita katika uchumi wa dunia pamoja na kupitia kwa wakati utekelezaji wa AfCFTA, Mifumo ya mtangamano wa biashara na uchumi wa kikanda na kati ya Kaskazini na Kusini mwa Dunia.
Vilevile, amebainisha kuwa
Warsha hiyo imeandaliwa na REPOA kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, Bunge la Afrika Mashariki (EALA) , EAC, CRDB, TradeMark Africa (TMA), Chama cha Kilimo cha Matunda na Mboga Tanzania (TAHA), na Korido la Ukuaji wa Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umaskini nchini (REPOA), Dkt. Donald Mmari amebainisha kuwa warsha hiyo inatarajiwa kuhudhuliwa na washiriki kati ya 150 hadi 200 kutoka Tanzania, Nchi Wanachama wa EAC, Jumuiya za Uchumi na Mashirika ya Maendeleo ya Kikanda na Bara la Afrika.
Aidha, Katibu Mkuu Msaidizi Bunhe la Afrika Mashariki Bw. Charles Ngeleja Kadonya amesema mapendekezo yote yatakayotokana na utafiti huo yatatekelezwa ipasavyo ili kuharakisha upanuzi wa biashara, ushindani na ukuaji wa uchumi shirikishi
Naye Meneja uhakiki ubora wa CRDB Kanda Arusha Bi Fatuma Abdul akiwa na Meneja Mkuu wa Maendeleo Chama cha Wakulima wa Maua, Matunda na mbogamboga (TAHA) Bw. Anthony Chamanga amesema warsha hiyo itasaidia kutatua changamoto na kuainisha fursa zilizopo na kuongeza mauzo nje ya nchi kwa kufuata viwango na ubora unaotakiwa wakati malipo ya mauzo hayo kuyanyika kwa urahisi.