Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

WAZIRI KAPINGA: SEKTA YA VIWANDA NA BIASHARA NI MUHIMILI MKUU WA UCHUMI WA TANZANIA


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema kuwa sekta ya viwanda na biashara ni muhimili muhimu katika uchumi wa Tanzania kutokana na mchango wake mkubwa katika Pato la Taifa, mapato ya ndani, pamoja na kuongezeka kwa mauzo ya nje.

Ameyasema hayo alipotembelea Ofisi ya Tume ya Ushindani (FCC), kwa lengo la kuona utendaji na utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo, Novemba 24, 2025, Jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa mikakati ya Serikali inalenga kuendeleza na kuongeza wigo wa viwanda nchini, kwani kupitia viwanda kutaimarisha ajira, kukua kwa mapato ya ndani na kupanuka kwa mauzo ya nje. Amebainisha kuwa Serikali itaendelea kutekeleza sera endelevu na kubuni sera mpya kila inapobidi kulingana na mabadiliko ya mazingira ya biashara ndani na nje ya nchi.

Waziri Kapinga amefafanua kuwa sekta ya viwanda na biashara ni sekta shirikishi inayoratibu shughuli na mipango na sekta nyingine nyingi, kwa lengo la kuboresha uratibu na kupunguza urasimu ili kufanya mazingira ya biashara kuwa rafiki kwa Wafanyabiashara, wawekezaji na Wajasiriamali wa Kitanzania.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha sera na kuongeza idadi ya viwanda vya uzalishaji ambavyo vitaongeza Pato la Taifa na mauzo ya bidhaa nje ya nchi. Kwa kuimarisha viwanda, amesema, uzalishaji wa malighafi utaongezeka na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa mapato ya nje.

Akizungumzia utendaji wa taasisi zilizo chini ya wizara, Waziri Kapinga amesema kunahitajika kuhakikisha taasisi hizo zinatekeleza majukumu yao kwa wakati na kwa ufanisi, kwa kuzingatia misingi bora ya kiutawala.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa, amesema tume hiyo inatarajia kuanzisha Baraza la Kitaifa la Utetezi wa Walaji, hatua ambayo inalenga kuimarisha ushiriki wa walaji na kuongeza udhibiti wa mwenendo wa biashara nchini. Amesema baraza hilo litaiwezesha FCC kusimamia vizuri zaidi waendeshaji wa biashara kama mamlaka ya ushindani na hivyo kushughulikia mahitaji ya walaji kwa ufanisi mkubwa. Bi. Ngasongwa amesisitiza kuwa lengo ni kuunda mfumo utakaowawezesha walaji kutetea maslahi yao ipasavyo sambamba na kuiwezesha tume kusimamia biashara kwa haki na weledi.