Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA ITATOA TUZO KWA WANAFUNZI WABUNIFU.


Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa kuanzia mwaka 2022 Wizara itatoa tuzo kwa mwanafunzi bora atakayebuni na kutengeneza kifaa, mfumo au nyenzo kinachoweza kutatua changamoto za kijamii.

 

Prof. Mkumbo amesema hayo leo Disemba 02, 2021 katika hafla ya utoaji tuzo na zawadi kwa wanafunzi bora katika kozi mbalimbali wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) wanaohitimu mwaka 2021

 

“Kuanzia mwaka 2022 Waziri wa Viwanda na Biashara atatoa tuzo kwa mwanafunzi aliyebuni na kutengeneza kifaa, mfumo au nyenzo kinachoweza kutatua changamoto za kijamii” alisema Prof. Mkumbo

 

Prof. Mkumbo amepongeza baraza la DIT kwa kuweka utaratibu wa mzuri wa kuwatambua wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi kwa kuwathamini na kuwapa zawaidi ili kuwahamasisha waliobaki kufanya vizuri zaidi ikiwa na kuonyesha ubunifu wao.

 

Aidha, Prof. Mkumbo amesisitiza kuwa tuzo itakayoanza kutolewa na Wizara itachochea ubunifu kwa wanafunzi na kuhamasisha wenye viwanda kuwafuata wahitimu katika taasisi hiyo kwa kuwa taasisi hiyo ina uwezo mkubwa wa kutoa wanafunzi wenye uwezo wa kufanya kazi viwandani.

 

 

Vile vile, Prof. ametoa wito kwa walimu wanapotoa elimu kwa wanafunzi wazingatie mwelekeo mpana wa nchi wa kisera ili mambo wanayoyabuni yaweze kujibu matakwa ya kisera, wakati huo huo chuo kiendelee Kubaki katika misingi na malengo ya uanzishwaji wake.

 

Naye Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Prof. Preksedis Ndomba amesema taasisi hiyo inatoa tuzo katika kila program kila mwaka kwa wanafunzi wa shahada na stashahada ambapo hupewa cheti na fedha ili kujenga ushindani na kuhamasisha juhudi kwa kila mwanafunzi.

 

 

Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Baraza katika chuo cha DIT, Dk Richard Masika amewataka wanafunzi hao kutumia akili, maarifa, ujuzi na uwezo walionao ili kubuni vitu mbalimbali vitakayoisaidia jamii na taifa kwa ujumla.