Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

WMA kuzingatia utii wa sheria, miongozo na kanuni mbalimbali zilizopo ili kuonngeza uadilifu na weledi kazini.


Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt.Hashil Abdallah ameitaka Menejimenti ya Wakala wa Vipimo (WMA) @wakalawavipimotanzania kutekeleza maono ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuzingatia utendaji kazi wenye weledi, ubora na viwango ili kupata matokeo chanya katika sekta ya biashara nchini.

Amesema hayo alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari Mjini Kibaha, mkoani Pwani baada ya kufungua kikao cha Menejimenti ya Wakala wa Vipimo (WMA) pamoja na kukabidhi magari mawili(2) ili kuboresha utendaji kazi na kuzindua Jarida maalum la Wakala lenye lengo la kupanua wigo wa uelimishaji na uhabarishaji umma kuhusu WMA.

Ili kuhakikisha maono hayo ya Rais Dkt Samia yanafikiwa, Dkt. Abdallah
ameitaka WMA kuzingatia mambo kadhaa ambayo ni pamoja na utii wa sheria, miongozo na kanuni mbalimbali zilizopo kwa kuongeza uadilifu na weledi kazini.

Ameielekeza Menejimenti kuondoa urasimu wa aina yoyote katika utendaji kazi huku akisisitiza kwamba Jarida alilozindua pamoja na kutoa habari mbalimbali za
Wakala, litumike kama nyenzo mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na wadau wa WMA hususani katika ufanyajibiashara.

Katika hatua nyingine, Dkt.Abdallah amempongeza na kumshukuru Rais Dkt Samia kwa kuendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa sekta mbalimbali za umma na kwa muktadha huo kwa WMA ambapo ametoa jumla ya magari 10 kwa Wakala hiyo ili kuboresha utendaji kazi.

Akizungumza kwa niaba ya Menejimenti nzima, Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA,Alban Kihulla amesema watatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu.
Kuhusu majukumu ya WMA
ambayo ndiyo haswa yaliyotolewa maelekezo kuongeza nguvu, Kihulla
amesema ni pamoja na uhakiki wa vipimo, ukaguzi wa vipimo pamoja na ukaguzi wa bidhaa zilizofungashwa kwa lengo la kukuza uchumi katika sekta mbalimbali.

Aidha, kuhusu magari waliyopokea, Mtendaji Mkuu ameishukuru Wizara na kukiri kuwa yatapunguza changamoto iliyopo lakini akaomba Wakala iendelee kufikiriwa kupatiwa mengine zaidi pamoja na vitendea kazi vingine mbalimbali ili kuboresha zaidi utoaji huduma kwa wananchi.