Habari
MAONESHO YA 50 YA SABASABA YAIMARISHA BIASHARA, UWEKEZAJI NA AJENDA YA "MADE IN TANZANIA"
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amesema Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yamedhihirisha mafanikio makubwa ya Tanzania katika kukuza uzalishaji, biashara na uwekezaji, huku yakifungua fursa mpya za masoko na ushirikiano wa kimataifa.
Ameyasema hayo Julai 13, 2026 katika kilele cha Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) na kubainisha maonesho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu linalowaunganisha wazalishaji, wafanyabiashara, wawekezaji, taasisi za fedha na wabunifu kutoka ndani na nje ya nchi, hatua iliyochangia kuibuka kwa mikataba mipya ya kibiashara na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali.
Amesema chini ya uongozi wa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kuboresha Sera, sheria na mifumo ya utoaji huduma ili kujenga uchumi unaoongozwa na sekta binafsi, jambo lililochochea ongezeko la uwekezaji, uzalishaji wa viwandani na ushiriki wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Kwa mujibu wa Kapinga, maonesho hayo pia yameonesha kuwa biashara ya kisasa haiwezi kutenganishwa na viwanda, teknolojia, viwango vya ubora, huduma za kifedha, usafirishaji na taarifa za masoko.
Amebainisha kuwa Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa zenye ushindani wa kimataifa, ikiwemo mazao ya kilimo yaliyoongezwa thamani, bidhaa za ngozi, nguo, mashine, vifaa vya ujenzi pamoja na ubunifu wa vijana na wanawake.
Waziri Kapinga amesema maadhimisho ya miaka 50 ya Sabasaba yameweka msisitizo mpya wa kuifanya ajenda ya "Made in Tanzania" kuwa nguzo ya maendeleo ya uchumi, akisisitiza kuwa bidhaa zinazozalishwa nchini zinapaswa kutambulika kwa ubora, usalama, uaminifu na ushindani ili ziendelee kupenya katika masoko ya dunia.
