Habari
LONDO- SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA UPIMAJI WA VIWANGO NCHINI
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo(Mb) amesema Serikali inaendelea kuimarisha huduma za upimaji nchini, huku ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na mataifa mengine pamoja na kutoa fursa kwa nchi hizo kutumia miundombinu iliyopo na Tanzania kunufaika na uwekezaji huo.
Ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kutembelea ujenzi wa Jengo la Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Jijini Mwanza, Septemba 09, 2026, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi na usalama wa miundombinu kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika ununuzi wa vifaa vya kisasa.
Aidha Londo amemtaka Mkandarasi wa jengo hilo kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo kwa wakati kwani kukamilika kwa jengo hilo litakalokuwa na ofisi pamoja na maabara mbalimbali litarahisisha utoaji wa huduma za maabara na utawala kwa wafanyabiashara wa kanda ya ziwa.
Hata hivyo ameitaka TBS kuhakikisha utekelezaji wa miradi na uwekezaji unaofanyika katika miundombinu unawanufaisha wananchi wa maeneo husika, ikiwemo kupitia upatikanaji wa huduma bora na kuongeza fursa za kiuchumi.
Vilevile Londo amelitaka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kutumia fursa zilizopo kushawishi jumuiya za kimataifa kuwekeza katika vifaa vya vipimo na teknolojia za kisasa katika maabara zilizopo nchini.
