Habari
UCHUMI SHINDANI UNAHITAJI TAASISI ZINAZOSIKILIZA NA KUTOA MAJIBU SAHIHI
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), amesisitiza kuwa ujenzi wa uchumi shindani unategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa taasisi za umma zinazosikiliza, kutoa majibu sahihi na kujirekebisha mara kwa mara ili kukidhi mahitaji ya wananchi na sekta binafsi.
Amebainisha hayo wakati wa kufunga Mkutano wa Kwanza wa Usuluhishi (Tanzania Ombudsman Forum 2026) Septemba 8, 2026 Jijini Arusha, ambapo amesema kuwa katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, taifa linalenga kujenga uchumi ulioimarika, wenye ushindani na unaojumuisha wote kupitia viwanda, teknolojia na uwekezaji.
Mhe. Londo alibainisha kuwa Mifumo madhubuti ya kushughulikia malalamiko ni nguzo muhimu ya ushindani wa kiuchumi. Inasaidia kubaini changamoto za utoaji huduma, kutatua kero kabla hazijawa kubwa, na kuimarisha uaminifu kwa taasisi za umma.
Aidha Londo alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wake Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa yanayofanyika kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha uaminifu kwa wawekezaji pamoja na kazi inayofanywa na Tume ya Rais ya kutathimini maboresho ya Kodi, akibainisha kuwa mapendekezo yake yanakwenda kuimarisha Taasisi ya Mshauri wa Walipa Kodi (Tax Ombudsman Service Tanzania) kupitia mfumo rasmi wa kisheria ili kuongeza haki na uwazi.
Mhe. Londo ametoa wito kwa Mshauri wa Walipa Kodi Tanzania kulifanya jukwaa hilo kuwa la kila mwaka ili kuendeleza mjadala, kujifunza, na kushirikiana katika kuboresha utoaji wa huduma za umma nchini.
Jukwaa hilo lilishirikisha wajumbe kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Afrika Kusini, Botswana, Nigeria, Pakistan, pamoja na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na washirika wa maendeleo.
