Habari
Afrika inapaswa Kuwekeza katika Elimu kwa Vijana kwa Maendeleo Endelevu

Rais Samia Suluhu Hassan amesema nchi za Afrika zinapaswa kuwekeza katika rasilimali watu hususan elimu kwa vijana ili kuwa na maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
Sambamba na hayo, amesema maendeleo ya bara la Afrika yatapatikana haraka iwapo wanawake na vijana watawezeshwa kwa mitaji na taasisi za fedha pamoja na kuwaondolea vikwazo vya kibiashara hasa katika maeneo ya mipakani.
Rais ameyasema hayo Septemba 12, 2022 wakati akifungua Mkutano wa siku tatu wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Mkutano huo wenye kaulimbiu “Wanawake na Vijana: Injini ya Biashara ya AfCFTA Barani Afrika” ni wa kwanza kufanyika tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika.
Alisema Afrika inahitaji nguvu kazi imara katika maendeleo ya kiuchumi hivyo uwekezaji katika elimu kwa vijana ni muhimu kwa kuwa sababu kubwa ya nchi nyingi zilizopiga hatua kimaendeleo ziliwaendeleza vijana kielimu.
Rais Samia alitoa mfano wa China ambayo alisema maendeleo yake yanachangiwa na kuwa na vijana wenye ujuzi hasa katika sayansi na teknolojia, hivyo nchi za Afrika hazina budi kuwekeza kwa vijana katika elimu ikiwamo ubinifu katika nyanja mbalimbali.
“China ni nchi ambayo inapigiwa mfano kwa maendeleo na siri kubwa ni uwekezaji iliyofanya ka vijana. Kampuni nyingi zinazofanya vizuri zinaongozwa na vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 pamoja na matumizi ya sayansi na teknolojia Afrika inaweza pia kujenga uchumi imara kwa kuwekeza zaidi kwa vijana katika elimu hasa sayansi. Kwa kufanya hivi tutapiga hatua kubwa kiuchumi,"alisema.