Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI KUENDELEA KUKUZA BIASHARA YA NDANI YA AFRIKA, VIWANDA NA USHINDANI CHINI YA AfCFTA


Serikali kuendelea kukuza Biashara ya ndani ya Afrika, kuendeleza Viwanda na kuongeza ushindani chini ya mfumo wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Aristides Mbwasi wakati akifungua kikao kazi cha Wataalamu cha Tathmini ya Utekelezaji wa
Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Februari 24, 2026 jijini Dar es Salaam.

Mbwasi ameleza kuwa tangu kuanza kushiriki katika Mpango wa Majaribio ya Ufanyaji Biashara (Guided Trade Initiative - GTI) Julai 2023, Tanzania imetoa zaidi ya Vyeti vya Uasili wa Bidhaa 500 kwa zaidi ya kampuni 40, huku mauzo ya bidhaa nje ya nchi chini ya AfCFTA yakiongezeka kufikia Dola za Marekani milioni 62.9 kwenda Ghana pekee, sambamba na kuongezeka kwa biashara katika nchi za Nigeria, Algeria na Misri.

Bidhaa kuu zilizouzwa nje ya nchi nipamoja na nyuzi za mkonge, kahawa, viungo na bidhaa za viwandani kama vioo (float glass), jambo linaloonesha hatua ya mabadiliko kuelekea uchakataji na ushiriki mkubwa wa sekta binafsi.

Aidha, Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kutekeleza mageuzi yanayolenga kuboresha mifumo ya forodha, kidijitali, urahisishaji wa biashara, na kupunguza vikwazo visivyo vya kiforodha (Non-Tariff Barriers - NTBs) ili kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na fursa za soko AfCFTA.