Habari
MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA WAWANUFAISHA WAKULIMA WA ZAO LA CHOROKO
Serikali imewataka wakulima na wafanayabiashara wa Mazao kuwa waaminifu na kuendelea kuunga mkono Mfumo wa Stakabadhi za ghala, huku ikiahidi kuimarisha upatikanaji wa pembejeo, mbegu, teknolojia za kisasa na masoko ya uhakika ili kuongeza tija katika mnyororo mzima wa thamani wa Mazao.
Vilevile, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) zinatakiwa kuwa na Mkakati wa kuwawezesha wakulima kuanzia hatua ya uzalishaji, ukusanyaji na uuzaji bora kupitia Mfumo wa Stakabadhi za ghala ili kuleta tija na ufanisi wa zao la choroko katika kupata soko la uhakika na bei nzuri.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, Februari 25, 2026, baada ya kushuhudia Mnada wa uuzaji wa zao la choroko kupitia Mfumo huo wa Stakabadhi za Ghala uliofanyika katika Ghala Teule la Ndilima Lililopo Hungumalwa mkoani Mwanza.
Waziri Kapinga pia amesema amefarijika kuona mafanikio yanayoonekana katika mnada huo wa choroko ambapo amebainisha kuwa Mwaka jana bei ya juu ya choroko ilikuwa shilingi 1,200 kwa kilo, mwaka huu 2025/26 imefikia shilingi 1,600 na hivyo kutekeleza maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), yaliyoahidi kuimarisha na kulinda Mfumo huo kwa manufaa ya mkulima na mfanyabiashara.
Naye, Mkurugenzi wa WRRB, Bw. Asangye Bangu, amesema utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika eneo la Kwimba na Kanda ya Ziwa ni hatua kubwa inayosaidia Wakulima kupata taarifa sahihi za bei, na ametoa rai kwa vyama vya Ushirika kuendelea kutoa elimu na kuweka mazingira rafiki kwa mkulima kupata fedha kwa wakati.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kwimba,Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija,amesema Mfumo wa Stakabadhi za Ghala umesaidia upatikanaji wa takwimu sahihi za mazao na kurahisisha upatikanaji wa soko.
Mbunge wa Jimbo la Sumve Mhe. Moses Bujaga, na Mbunge wa Jimbo la Kwimba Mhe. Cosmas Bulala Wamesema zao la choroko ni zao la kibiashara na mbadala wa zao la pamba kwa wakazi wa majimbo hayo hivyo wameomba kuangaliwa kwa tozo zisizo za lazima ili kuongeza tija kwa mkulima.
