Habari
SERIKALI KUIMARISHA USHIRIKIANO WA SEKTA BINAFSI KATI YA TANZANIA NA SINGAPORE KUKUZA BIASHARA
Serikali ya Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi ya Tanzania
na Shirikisho la Biashara la Singapore kama mkakati wa kukuza kiwango cha
biashara baina ya mataifa hayo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Denis Londo (Mb), wakati
akizungumza na Balozi wa Singapore nchini Tanzania, Mhe. Balozi Douglas Foo Februari 23, 2026 jijini Dar es Salaam.
Londo alisema ushirikiano huo utasaidia kukuza biashara na uwekezaji, hasa biashara ndogo na za kati.
Alisema Singapore imepiga hatua kubwa kiuchumi na nafasi yake kama kitovu cha kimataifa cha biashara, fedha, vifaa na uvumbuzi yanaendelea
kuhamasisha nchi nyingi zinazoendelea.
Naye Balozi Foo alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika sekta za kimkakati zikiwemo maendeleo ya viwanda na maeneo maalum ya kiuchumi, miundombinu kupitia ubia wa sekta ya umma na binafsi (PPP), uzalishaji wa dawa na vifaa tiba, uongezaji thamani katika sekta ya madini, pamoja na kilimo na usindikaji wa mazao. Aidha, alitaja pia fursa zilizopo katika sekta za utalii, usafirishaji na uchumi wa kidijitali.
