Habari
WANAMICHEZO WA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA TIMAMU KWA USHINDI - SHIMIWI 2025 MWANZA

Wachezaji wa timu ya Wizara ya Viwanda na Biashara wamejiandaa sawasawa na kuahidi kuendelea kuitangaza vema Wizara hiyo pamoja na Taasisi zake, huku wakihimizwa kufanya vizuri katika michezo yote watakayoshindana katika Mashindano hayo ya 39 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika jijini Mwanza kuanzia Septemba 1 hadi 16, 2025.
Akizungumza wakati wa kuwaaga wachezaji hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah amesema ameiandaa vema timu za michezo yote na hana wasiwasi kwani mwaka huu ni mwendo wa ushindi na amewaaga wachezaji hao Agosti 27, 2025 baada ya kufanya mazoezi ya kutosha kwa muda mrefu.
"Nikiwa 'captain' wa timu ya mpira wa miguu na mwanamichezo kwelikweli, sina wasiwasi na wachezaji wote. Ninahakikisha mnasafiri vizuri, mnakaa kambini Mwanza vizuri na nawategemea muitangaze vema Wizara yetu ya Viwanda na Biashara " amesema Dkt. Abdallah.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi na Utawala wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Saidi Msabimana amewatakia kila la kheri wachezaji hao kuahidi kuendelea kuwaandalia mazingira bora ya kimichezo. Aidha, amewashauri watumishi webgine waliobakia ofisini kuendelea kujiandaa na maziezi ya mara kwa mara kwani mwakani wataenda watumishi wengine na wale walioenda mwaka huu, watawapisha ambao hawakuenda. Michezo ni haki ya kila mtumishi kushiriki lakini hatuwezi kufunga ofisi kwa sababu ya wote kwenda Mwanza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya michezo ya wizara hiyo, Bw. Pius Mpinzile amewahakikishia viongozi kuwa timu imejiandaa vizuri na inatumaini kufanya vizuri zaidi na kuibuka washindi.