Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

BRELA Yatakiwa Kuboresha Utoaji wa Huduma kwa TEHAMA


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeiagiza Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa kutumia mifumo ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji kwa kutoa huduma bora za usajili na utoaji leseni kwa wananchi kwa haraka na kwa gharama nafuu.

 Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Japhet Hasunga (Mb) wakati wa kikao cha Kamati hiyo katika kupitia na kuchambua Taarifa ya Ukaguzi wa Ufanisi kuhusu Usimamizi wa Shughuli za Usajili wa Biashara na Utoaji wa Leseni kilichofanyika Oktoba 26, 2022 Bungeni Dodoma.

 Aidha, Wajumbe wa Kamati hiyo walitoa maoni na mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma za usajili na utoaji leseni kwa kutumia mifumo ya TEHAMA hususani katika kuhakikisha mifumo ya Taasisi nyingine inayohusu taarifa za usajili iweze kuongea na kubadilishana taarifa na kuhakikisha kuwa mfumo wa Usajili wa BRELA unafanya kazi pamoja na Mfumo wa Dirisha moja la Uwekezaji

Akijumuisha maoni na mapendekezo ya Wajumbe wa Kamati hiyo, Kaimu Katibu Mkuuwa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bw. Ally Gugu amesema Wizara itayafanyia kazi maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa ili kuhakikisha kuwa BRELA inaendelea kuboresha utoaji wa huduma zake kwa kutumia mifumo ya TEHAMA ili kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara wa ndani na nje wenye nia ya kuwekeza na kufanya biashara nchini.

 Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa amesema Mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao (ORS) tangu ulipoanza kutumika mwaka 2018 umekuwa ukitoa huduma mbalimbali za usajili wa majina ya biashara, makampuni, alama za biashara, utoaji wa hataza, utoaji wa leseni za biashara, leseni za viwanda na usajili wa viwanda vidogo. Aidha, Nyaisa ameongeza kuwa Mifumo hiyo ya TEHAMA umerahisisha utendaji kazi kwa BRELA na upatikanaji wa huduma za usajili na utoaji leseni kwa haraka na gharama nafuu kwa wananchi na hivyo kukiza biashara na uchumi kwa ujumla