Waziri wa viwanda na Biashara, Mhe.Dkt. Suleimani Jafo (Mb) amewashauri wafanyabiashara nchini kuchangamkia masoko ya kimataifa na kutengeneza uchumi wao kupitia Biashara za mipakani.
Pia amewataka kuhakikisha wanaongeza ubora wa bidhaa wanazozizalisha na kuongeza thamani ili kuweza kumudu ushindani wa soko la kimataifa.
Jafo ameyasema hayo Mei 3, 2025 jijini Arusha katika jukwaa la kiuchumi mkoa wa Arusha lililoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Mhe.Dkt.Jafo amesema kuwa Tanzania imekuwa ikifanya juhudi kubwa kufufua Viwanda na kuvutia wawekezaji wa viwanda hivyo ni fursa kwa watanzania kuwekeza na kuchakata bidhaa zenye ubora na kuchangamkia fursa za masoko ya ndani na nje.
Dkt. Jafo amesema kuwa amepata ujasiri huo baada ya Serikali ya Tanzania kukutana na nchi ya Malawi kumaliza changamoto iliyokuwa imejitokeza na kusababisha zuio la uingizaji wa bidhaa za kilimo baina ya nchi hizo mbili.
Amesema Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa hasa kwa upande wa biashara kwa kutanua masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Nataka niwaambie ndugu zangu jana tulikuwa na kikao Tanzania na wenzetu wa Malawi kuondoa mambo yote yaliyokuwa yanaonekana ni changamoto kama hapa Arusha kuna wafanyabiashara wanaofanya biashara na Malawi, jana jambo hilo tumelimaliza kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, nendeni mkafanye biashara kwa upana unaotakiwa tutengeneze fedha nchi isonge mbele,”amesema Dkt. Jafo
Malawi na Afrika Kusini zilizuia shehena ya ndizi kutoka Tanzaniia kuingia kwenye nchi hizo ambapo baadaye Tanzania nayo ilipiga marufuku kwa bidhaa za kilimo kutoka nchi hizo, uamuzi ambao ulianza kuathiri wafanyabiashara wa mazao mbalimbali ya kilimo.
Baada ya siku mbili za utekelzaji wa zuio kwa bidhaa za kilimo kutoka nchi hizo mbili, Serikali ya Tanzania iliondoa zuio hilo kupisha majadiliano.
Waziri wa Kilimo, Mhe Hussein Bashe, Aprili 23 , 2025 alitangaza kuanza utekelezaji wa zuio kwa bidhaa hizo baada ya Aprili 17, 2025 kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii kueleza ifikapo siku hiyo Serikali ya Tanzania itazuia uingizaji wa mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka mataifa hayo