Habari
SERIKALI YAJIDHATITI KUJENGA UCHUMI JUMUISHI,SHINDANI NA IMARA-LONDO
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imejidhatiti kujenga uchumi shindani, jumuishi, na imara na kusisitiza dhamira yake ya kuongeza tija katika viwanda, kupanua wigo wa biashara, kukuza sekta binafsi, na kuvutia uwekezaji mkubwa zaidi.
Mageuzi mbalimbali yanaendelea kutekelezwa ili kuboresha mazingira ya biashara nchini, hatua inayolenga kuziwezesha kampuni za ndani kushiriki kikamilifu katika masoko ya kikanda na kimataifa, huku ikitambua sekta binafsi kama injini kuu ya ukuaji endelevu na uzalishaji wa ajira.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dennis Londo (Mb) wakati wa utoaji wa Tuzo za Kampuni Bora ya Mwaka Barani Afrika 2026 (ACOYA 2026) yenye kaulimbiu ya, “Afrika Moja, Soko Moja, Bidhaa za Kimataifa,” Juni 12,2026 Jijini Dar es Salaam.
Aidha Mhe Londo alibainisha kuwa maono hayo yanaenda sambamba na matarajio ya bara la Afrika kuelekea mtangamano wa kiuchumi, Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA) lilitajwa kama fursa ya kihistoria itakayofungua uwezo kamili wa soko lenye zaidi ya watu bilioni 1.4.
Aidha Mhe. Londo aliyahimiza Mataifa ya Afrika kuchangamkia fursa ili kuimarisha minyororo ya thamani ya kikanda, kuongeza kasi ya maendeleo ya viwanda, na kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wa Kiafrika wanakuwa wanufaika wakuu wa mabadiliko haya ya kiuchumi na ikiwa Tanzania kuwa katika nafasi ya kimkakati ya kuunga mkono maono hayo kutokana na miundombinu yake inayozidi kupanuka inayotoa msingi madhubuti wa kukuza biashara ya kikanda na kibara.
Vilevile amesema Serikali inaendelea kufanya kazi kwa karibu na sekta binafsi ili kuifanya Tanzania na Afrika kuwa msambazaji wa malighafi na kuwa kitovu kinachozalisha bidhaa, huduma, na teknolojia za daraja la kwanza zinazoheshimika duniani kote na kuweka mazingira wezeshi yanayochochea ubunifu, uongezaji thamani wa bidhaa, na ukuaji wa mauzo ya nje.
Aidha Londo amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili kuwazeesha wanawake na vijana, na kuunga mkono viwanda vinavyoongeza thamani ya rasilimali za ndani ili kutengeneza ajira zenye tija.
