Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

WAZIRI KAPINGA ATEMBELEA MAANDALIZI YA SABASABA, ATAKA MAONYESHO YAWE NA MVUTO ZAIDI


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, ametembelea na kukagua maendeleo ya maandalizi ya Maonyesho ya Biashara ya (Sabasaba) yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, akisisitiza umuhimu wa kuyaandaa kwa kiwango kikubwa ili yaweze kuvutia washiriki na wageni wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi.

Akizungumza Juni 13, 2026 mara baada ya ziara hiyo, Mhe. Kapinga amesema kuna haja ya kuandaa maudhui ya video yatakayoonyesha shughuli za kampuni na taasisi zao pamoja na teknolojia wanazotumia, ili kuongeza mvuto kwa wageni watakaotembelea mabanda mbalimbali wakati wa maonyesho hayo.

Amesema Sabasaba si shughuli ya TANTRADE pekee bali ni ya taifa zima, hivyo inahitaji ushirikiano wa wadau wote kuhakikisha inakuwa kubwa na yenye mafanikio zaidi, aidha ameipongeza sekta binafsi kwa kuwa na bidhaa bora na mashine za kisasa, huku akieleza matarajio yake ya kuona maonyesho hayo yakiwa jukwaa la kuonesha ubunifu, teknolojia na bidhaa zenye kuvutia zaidi kwa manufaa ya maendeleo ya biashara nchini.