Habari
Wafanyabiashara nchini kutumia zaidi Maabara za Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Biashara Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt.Hanifa Mohamed ametoa rai kwa wadau na wafanyabiashara nchini kutumia zaidi Maabara za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kupata bidhaa zenye ubora zaidi.
Amebainisha hayo wakati akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.Hashil Abdallah katika ziara ya kutembelea Maabara za Uhandisi Ujenzi katika Shirika hilo Julai 04,2025 Jijini Dar es Salaam.
Dkt.Hanifa amesema kuwa ziara hiyo imewafanya kuona Serikali inavyoendelea na uwekezaji mkubwa katika Vifaa vya vipimo ambavyo vinatumika kupimia bidhaa na vifaa mbalimbali vya ujenzi katika Maabara hizo hivyo ni vyema wadau wake kutumia fursa hiyo kwani mpaka sasa kuna baadhi ya vipimo bado havijaanza kutumika kwa kukosa vifaa vya kupima ikiwemo mabomba ya maji ya milimita 800.
Nae Mkurugenzi Mkuu Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt.Ashura Katunzi amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kuwaonesha viongozi hao kuifahamu shirika na kuona uwezo mkubwa wa Maabara hizo za vifaa ujenzi na miundobinu ya maji zinavyofanya kazi kwa ubora mkubwa.
Vilevile Dkt. Katunzi ameshauri kuwa wenye Mamlaka ya kusimamia mindombinu watumie Maabara za TBS kuhakikisha vifaa na huduma zinakuwa na ubora kutokana na mikataba yao waliongia.