Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

CHINA YAONGEZA FURSA ZA SOKO KWA BIDHAA ZA TANZANIA


Serikali imesema uamuzi wa China kuondoa ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazotoka Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika utatoa fursa kubwa kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa ndani kuongeza mauzo katika moja ya masoko makubwa duniani.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Dennis Londo (Mb), Julai 06, 2026 wakati wa maadhimisho ya ‘China Day’ yaliyofanyika katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Londo amesema ushirikiano wa Tanzania na China umeendelea kuimarika kwa miaka mingi na umechangia ukuaji wa sekta ya viwanda, maendeleo ya miundombinu, uhamishaji wa teknolojia, ukuzaji wa ujuzi na ajira, hatua zinazochochea maendeleo ya uchumi wa nchi.

Amesema fursa ya kuuza bidhaa bila ushuru inapaswa kutumiwa kuongeza mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani badala ya malighafi pekee, akieleza kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi za kilimo, madini, mifugo, uvuvi na maliasili zinazoweza kuzalisha bidhaa zenye ubora wa kimataifa.

Aidha, amewahimiza wawekezaji kuwekeza zaidi katika viwanda vya kuchakata mazao, uzalishaji, ufungashaji, uwekaji chapa na mifumo ya kuhakikisha ubora wa bidhaa ili kuongeza ushindani katika soko la China.

Londo amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, huku ikiimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa, mifumo ya kidijitali, utafiti, ubunifu, akili bandia na nishati jadidifu ili kuongeza uwezo wa uzalishaji nchini.

Pia amewataka wafanyabiashara wa Tanzania kutumia kikamilifu fursa hiyo kwa kuboresha ubora wa bidhaa zao, kuzingatia viwango vya kimataifa na kujenga ushirikiano wa kibiashara na wawekezaji pamoja na wanunuzi kutoka China.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na China ili kufungua fursa zaidi za biashara na uwekezaji kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.