Habari
MWANAMKE NI INJINI YA UCHUMI WA TANZANIA- LONDO
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb) akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amewataka wanawake nchini kutoka kwenye fikra za kufanya biashara za kawaida za kujikimu na badala yake kuelekeza nguvu zao katika umiliki wa viwanda na uzalishaji wenye tija unaolenga masoko ya kimataifa.
Amebainisha hayo wakati akifungua rasmi maadhimisho ya miaka 10 ya jukwaa la Malkia wa Nguvu 2026 (Kanda ya Morogoro) Agosti 28,2026 ambapo amesema miaka 10 ya jukwaa hilo imethibitisha kuwa mwanamke akipewa nafasi na kuwezeshwa kiuchumi, anakuwa nguvu kuu na injini ya mabadiliko kwa familia, jamii na Taifa kwa ujumla.
Akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu ya “Koleza Levels,” Mhe. Londo alieleza kuwa ni wito mzito unaomtaka kila mwanamke kuongeza kasi, ubora na thamani katika kila sekta anayojihusisha nayo na kusiaiatiza ujumbe huo unalenga kumtoa mwanamke kutoka kuuza bidhaa za kawaida hadi kuingia kwenye uzalishaji mdogo, na hatimaye kumiliki viwanda vinavyoweza kutawala masoko ya Afrika na dunia.
Aidha, Naibu Waziri huyo alibainisha kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara imeweka mazingira wezeshi, sera bora na miundombinu rafiki itakayomvusha mwanamke kutoka kuwa mlaji au mwagizaji wa bidhaa za nje, na kuwa mzalishaji mkuu anayeongeza thamani ya rasilimali za ndani.
Mhe. Londo aliwasihi wanawake kutohofia kuanza biashara na mtaji mdogo, akibainisha kuwa aibu si kuanza na kile ulichonacho, bali ni kuwa na fursa na wazo lakini kusita kuchukua hatua.
Katika hatua nyingine, alihimiza uimarishwaji wa kampeni ya “Buy Tanzania” kama njia kuu ya kujenga uchumi unaojitegemea, huku akiwataka wazalishaji kuhakikisha bidhaa zao zina ubora wa juu na vifungashio vya kisasa ili kuhimili ushindani. Mhe. Londo aliutaja Mkoa wa Morogoro kuwa na fursa za kipekee za kimkakati kutokana na ardhi yenye rutuba na mtandao mzuri wa kijiografia, hivyo aliwataka wanawake wa mkoa huo kutoishia kwenye masoko ya ndani tu bali kuvuka mipaka.
