Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

UJENZI WA MAABARA ZA VIPIMO DODOMA NI CHACHU YA KUKUZA BIASHARA NA VIWANDA KANDA YA KATI


Ujenzi wa jengo jipya la Ofisi na Maabara za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) jijini Dodoma ni mkombozi wa kiuchumi kwa Kanda ya Kati. Uwekezaji huu wa ghorofa tano utahudumia zaidi ya viwanda 300, hatua itakayorahisisha usafirishaji wa sampuli kutoka milia ya kanda ya Kati na mingine iliyokaribu, kupunguza gharama za uendeshaji, na kuongeza ufanisi katika kurasimisha biashara na kukuza ubora wa bidhaa nchini.

Hayo yamebainishwa Machi 25, 2026, na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga (Mb), akiwa ameambatana na Naibu Waziri Mhe. Dennis Londo (Mb), Kaimu Katibu Mkuu Bw. Needpeace Wambuya, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu: Bw. Said Msabimana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara: Bw. Sempeho Manongi
alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Jengo hilo uliokamilika kwa 94%.

Aidha, Waziri Kapinga amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi huo ambao ni kielelezo cha mpango mkakati wa taasisi hiyo kuwa na majengo ya kisasa yanayoendana na mahitaji ya sasa.

Ameeleza kuwa lengo la Wizara ni kuona taasisi muhimu kama TBS zinafikika kwa urahisi ili kuwafikia wananchi kwa haraka na kuwezesha uendelevu wa biashara zao na kuagiza kuongeza kasi ya ujenzi wa Ofisi ya Mwanza na kuanza kwa mchakato wa Ofisi ya Arusha ili kutekeleza Dira ya Maendeleo ya 2050 kwa kuzingatia thamani ya fedha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, amesema jengo hilo linatarajiwa kuzinduliwa wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya TBS. Amesema uwepo wa maabara za kisasa jijini Dodoma utasaidia mikoa ya Iringa, Singida, na mikoa jirani kupata majibu ya vipimo kwa haraka, jambo litakaloongeza tija kwa wadau wa viwanda na wananchi kwa ujumla.

Jengo hili litakuwa kituo muhimu cha kutoa huduma za kiufundi na kukuza viwango, likiwa na maabara za kutosha kuhudumia mahitaji ya kanda hiyo.