Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

NAIBU KATIBU MKUU BW. ARISTIDES MBWASI ASHUHUDIA KUSAINIWA KWA MIKATABA KATI YA BENKI YA CRDB NA PROPARCO JIJINI NAIROBI


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Aristides Mbwasi ameshuhudia kusainiwa mikataba miwili ya makubaliano ya hati ya dhamana kati ya Benki ya CRDB na Shirika la Fedha la Ufaransa la Proparco kando ya Mkutano wa Afrika na Ufaransa, Africa Foward Summit unaoendelea Mei 11, 2026 katika jiji la Nairobi, Kenya.

Mkataba wa kwanza ambao ni mkubwa zaidi katika dhamana ambazo zimewahi kutolewa na Shirika hilo wa Euro Milioni 50 unalenga kusaidia uwezeshaji wa wajasiriamali wadogo na wakati nchini hususan biashara changa za vijana na biashara zinazoongozwa na wanawake.

Mkataba wa pili wenye thamani ya Euro Milioni 40 unalenga kuchochea biashara za kikanda kwa kuwawezesha wafanyabiashara katika masoko ambayo Benki inatoa huduma Tanzania , Burundi na DRC kukuza biashara zao na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi.

Akizungumza katika hafla ya kusaini mikataba hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela amesema benki inajivunia kuendeleza ushirikiano na Proparco, huku akibainisha kuwa hii ni fursa nzuri kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kukuza biashara zao.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Proparco, Françoise Lombard amesema ushirikiano na Benki ya CRDB umekuwa na manufaa makubwa sana na wanaamini mikataba hii mipya itakwenda kusaidia zaidi kuwawezesha wajasiriamali wengi katika masoko ambayo Benki inayahudumia.

Mkutano wa Africa Foward unayakutanisha mataifa mbalimbali ya Afrika na Ufaransa ambapo ujumbe wa
Tanzania umeongozwa na Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.