Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

YIWU MARKET NCHINI KUONGEZA BIASHARA KATI YA TANZANIA NA CHINA


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Aristides Mbwasi amesema ujio soko jipya la YIWU Market ndani ya Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo, Dar es Salaam, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Tanzania na China.

Amesema hayo akimwakilisha Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Dennis Londo (Mb) katika uzinduzi wa Soko hilo lililopo katika kituo hicho cha EACLC , ambapo amesema uzinduzi huo unatekeleza dhamira ya viongozi wa mataifa hayo mawili ya kuendelea kukuza biashara, uwekezaji na diplomasia ya uchumi.

Mbwasi amesema Serikali imepongeza maendeleo makubwa ya EACLC tangu ilipozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akibainisha kuwa kituo hicho kimeendelea kuvutia wafanyabiashara kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali ambapo zaidi ya maduka 190 yamepangishwa.

Ameongeza kuwa soko hilo litawasaidia wafanyabiashara wa Tanzania kupunguza gharama za safari za China kutafuta bidhaa, badala yake zitapatikana nchini na kusisitiza bidhaa zote zinazouzwa hapo zinakidhi viwango vya ubora vilivyothibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kulinda maslahi ya watumiaji.

Aidha amesema soko hilo limeandaa eneo maalumu la Made in Tanzania, litakalotumika kutangaza na kuuza bidhaa zinazozalishwa nchini katika soko la China na mataifa mengine kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), hatua hiyo inatarajiwa kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi, ikiwemo mazao ya kilimo kama ufuta na soya ambayo tayari yanapata soko nchini China.

Ameongeza kuwa YIWU Market siyo fursa kwa Tanzania pekee bali kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki, SADC na Soko Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), ambapo Dar es Salaam inatarajiwa kuwa kitovu cha biashara za kikanda. Alibainisha kuwa kituo hicho kina huduma mbalimbali za taasisi za Serikali, ikiwemo TRA, zinazorahisisha uingizaji na usafirishaji wa bidhaa, hivyo kuongeza ufanisi wa biashara na uwekezaji.