Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI YAWAKARIBISHA WAWEKEZAJI WA VIWANDA KONGANI YA KWALA


Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Salum Waziri, amewakaribisha wawekezaji katika sekta ya viwanda biashara wa ndani na nje ya nchi kuwekeza nchini hususani Kongani ya Viwanda ya Kwala inayotarajiwa kuwa miongoni mwa maeneo makubwa ya viwanda barani Afrika.

Vilevile amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira bora na wezeshi ya biashara ikiwemo kukamilisha miundombinu muhimu ya gesi, Reli ya Kisasa (SGR) na barabara ili kuongeza ufanisi wa uwekezaji na usafirishaji katika eneo hilo na itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazijitokeza viwandani kwa kuunda timu maalumu huku masuala makubwa yakipelekwa kwa Waziri wa Viwanda na Biashara

Balozi Waziri ameyasema hayo Julai 16, 2026 wakati wa ziara yake katika Kiwanda cha King Lion na Kongani ya Viwanda ya Kwala Mkoani Pwani kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji na kusikiliza na kutatua changamoto zinazojitokeza katika viwanda hivyo.

Aidha, ameongeza kuwa uwekezaji mkubwa uliopo katika Viwanda hivyo inaonesha dhamira ya Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda na mazingira mazuri na rafiki ya biashara yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya Kibaha Mhe. Nickson John amesema Kongani ya Kwala inatarajiwa kuwa kitovu kikubwa cha viwanda nchini, ambapo mradi huo ukikamilika utakuwa na viwanda 250 na kuzalisha ajira zaidi ya 50,000 kwa vijana pamoja na kuongeza mapato ya Halmashauri.

Aidha amebainisha kuwa mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu muhimu inayowezesha shughuli za viwanda na biashara katika kujenga barabara zinazoingia eneo la viwanda, inaendelea na maandalizi ya mradi wa maji wenye thamani ya Sh bilioni 20 na tayari imetekeleza mradi wa umeme wa Sh bilioni 3 ili kuhakikisha mazingira bora ya uwekezaji.