Habari
Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) asema ndani ya mwaka mmoja, mifuko na program za uwekezaji wananchi kiuchumi imetoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 713.8

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema ndani ya mwaka mmoja, mifuko na program za uwekezaji wananchi kiuchumi imetoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 713.8 ili kukuza ushiriki wa wananchi kwenye shughuli za kiuchumi katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi, 2023.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo Bungeni Dodoma Mei 04, 2023 wakati wa kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2023/24 ambapo Wizara imeliomba Bunge kupitisha bajeti ya zaidi ya Sh bilioni 119.018 kati ya hizo Sh 43.566 kwa ajili ya maendeleo na Sh bilioni 30.347 ni fedha za ndani na Sh bilioni 13.22 ni fedha za nje.
Aidha, Dkt. Kijaji alisema kuwa uchambuzi wa mikopo hiyo unaonesha jumla ya ajira 3,122,104 zilizalishwa, kati ya ajira hizo, wanawake ni 1,623,494 sawa na asilimia 52 na wanaume ni 1,498,610 sawa na asilimia 48.
Mikopo hiyo imetolewa kwa wajasiriamali 2,203,838 na kati yao wanawake ni 1,234,149 sawa na asilimia 56 na wanaume 969,689 sawa na asilimia 44 katika sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi. Amesema Dkt. Kijaji.
Aidha, Dkt. Kijaji alisema pia katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Machi, 2023, Wizara kupitia Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Wajasiriamali Wananchi (NEDF) imetoa jumla ya mikopo 1,474 na kati ya hao wanawake ni 668 sawa na asilimia 45.3 na wanaume ni 806 sawa na asilimia 54.7 yenye thamani ya Sh bilioni 3.50 ambapo mikopo 516 sawa na asilimia 35 yenye thamani ya Sh bilioni 1.225 ilitolewa kwa miradi ya vijijini.
Dkt. Kijaji pia alisema mikopo hiyo iliweza kuzalisha ajira 5,489 ambapo wanawake ni wanawake 2,668 sawa na asilimia 48.6 na wanaume ni 2,821 sawa na asilimia 51.4.
Alisema pia Wizara imeweza kuwaungisha wajasiriamali 13 ambao walipata mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 1.151 kupitia Benki za Azania na CRDB ambapo jumla ya ajira 259 zimezalishwa.
Dk Kijaji alisema Wizara imeendelea kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya utendaji wa Mifuko na Programu za Uwezeshaji. Katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Machi, 2023, Wizara imefanya tathmini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa lengo la kupima matokeo ya utendaji wa huo katika kupunguza mzunguko wa umaskini katika jamii.
Akifafanua Dkt. Kijaji alisema matokeo yanaonesha kuwa kaya 1,965,743 zimetambuliwa kati ya kaya hizo, kaya 1,283,266 zilikidhi vigezo na kupatiwa ruzuku; kuwezesha watu 1,236,945 kupata ajira za muda mfupi, kuwezesha jumla ya watoto 1,280,779 kutoka katika kaya maskini kuhudhuria masomo na kupunguza kiwango cha umaskini uliokithiri kwa asilimia 8 na kiwango cha umaskini wa kaya kumudu gharama za mahitaji ya msingi kwa asilimia 10.