Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

DKT. KIJAJI AWAAGIZA WAZALISHAJI, WASAMBAZAJI NA WAFANYABIASHARA KUSHUSHA MARA MOJA BEI YA VIFAA VYA UJENZI.


Waziri wa Uwekezaji,  Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amewataka wazalishaji wa vifaa vya ujenzi, wasambazaji na wafanyabiashara kushusha mara moja Bei ya bidhaa hizo walizopandisha kiholela bila sababu za msingi ambayo imepelekea kumuumiza mlaji wa chini.

Agizo hilo ni matokeo ya tathimini iliyofanyika ambayo ilibaini kuwa ongezeko holela la bei ya vifaa vya ujenzi  hususani saruji na nondo ambalo linasababishwa na wazalishaji wa bidhaa husika kufanya uzalishaji na kutokuwa na mfumo wa wazi.

Waziri Kijaji aliyasema hayo Leo tar. 7 Februari, 2022 Jijini Dodoma wakati alipokuwa akiongea na vyombo vya Habari ambapo pia alisema agizo hilo pia  linawahusu wazalishaji na wasambazaji wa vinywaji baridi.

Alisema kuwa tathimini ilijiridhisha kuwa gharama halisi za uzalishaji wa saruji haiakisiwi katika bei ya saruji iliyopo sokoni ikilinganishwa na uwiano huo katika Nchi jirani, na kwamba ongezeko la Bei ya saruji na nondo halina uwiano halisi na gharama za usafirishaji na usambazaji.

"Utafiti wetu umegundua kuwa Kuna ucheleweshaji wa makusudi wa utoaji saruji kutoka viwandani kwenda kwa wasambazaji na wanunuzi wa ndani hususani wale wasambazaji na wanunuzi wadogo ambao tayari wanakuwa wamekwisha lipia saruji husika na kuweza kusababisha wao kupandisha bei " Alisema Dkt. Kijaji.

Aidha kupitia utafiti huo ametoa maagizo kwa mamlaka zote za udhibiti kuchukua hatua kali dhidi ya walimbikizaji na wauzaji kupitia mlango wa nyuma (black market) wanaosababisha bei za bidhaa sokoni kupanda  ili kuhakikisha bidhaa zinafika sokoni kwa wakati na kwa bei shindani ambayo haina maumivu kwa wananchi.

"Kwa kuwa kitendo cha kupanga bei kati ya washindani ni uhujumu uchumi nawaagiza mamlaka husika kuchukua hatua kali dhidi ya wote wataobainika kukaa na kupanga bei ya bidhaa kwa mujibu wa sheria za Nchi yetu"

"Ninawaelekeza wazalishaji kuzalisha bidhaa hizo kulingana na uwezo uliosimikwa kwenye viwanda vyenu ili kukidhi mahitaji ya Soko ndani ya Taifa letu na kuwa na uwezo wa kuuza nje ya mipaka yetu ." Alisema Dkt. Kijaji

Pia wazalisha wa vifaa vya ujenzi kuhakikisha wanaweka mifumo mizuri ya usambazaji wa vifaa ili Kuzuia kupanda kwa bei huku akiwataka maafisa biashara wa Mikoa na Wilaya kote Nchini kufuatilia kwa karibu mwenendo wa Bei za bidhaa kwenye maeneo yao na kuwasilisha taarifa mara kwa mara.

Hata hivyo alisema Serikali ina wajibu wa kidhibiti mienendo hadhaifu na kandamizi ya wazalishaji wa bidhaa, biashara kwenye soko ikiwa ni pamoja na upandishaji holela wa Bei zote nchini huku mwenye nia ovu ya kumkandamiza mwananchi kuchukuliwa hatua.