Dkt.Mwinyi mgeni rasmi ufunguzi wa 49 ya DITF Julai 7, 2025
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt.Selemani Jafo amesema kuwa
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), Julai 7, 2025 katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba), Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Waziri Jafo ameyasema hayo Julai 2, 2025 wakati akiongea na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam.
Maonesho haya, yanayoandaliwa kila mwaka na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), yalianza rasmi tarehe 28 Juni 2025 na yanatarajiwa kufungwa tarehe 13 Julai 2025.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni Tanzania: Lango la Biashara ya Kikanda na Kimataifa ikilenga kukuza ushirikiano wa kibiashara baina ya Tanzania na mataifa mengine kupitia uwekezaji, viwanda na teknolojia.
Jafo amesema maonesho ya mwaka huu yamevutia washiriki kutoka ndani na nje ya nchi, na kuthibitisha umuhimu wake kama jukwaa kuu la kukuza Biashara na Diplomasia ya kiuchumi.
"Tumefikia zaidi ya asilimia 97 ya malengo ya ushiriki, ambapo kampuni 3,501 kutoka ndani ya nchi zimesajiliwa. Aidha, kampuni 394 kutoka nje ya nchi nazo zimeshiriki, na kufanya jumla ya washiriki kufikia 4,040," alisema Dkt. Jafo.
Aliongeza kuwa, serikali inaendelea na juhudi za kuimarisha utambulisho wa bidhaa za Tanzania kwa kuzindua alama maalum kama ‘Tanzania Honey Brand Mark’, pamoja na maandalizi ya alama ya kitaifa *Made in Tanzania*, itakayosaidia bidhaa za ndani kupata soko la kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Bi Latifa Khamis, alisema mwaka huu kumekuwa na ongezeko kubwa la ushiriki, huku baadhi ya waombaji wakiendelea kujisajili kupitia mfumo wa mtandaoni.
Bi.Latifa alisema kwenye maonesho kutakuwa na proogramme mbalimbali zikiwepo siku ya nchi mbalimbali kuonyesha bifhaa zao pamoja na kufamya mikutano ya Biashara.
Mgeni rasmi katika kuhitimisha maonesho hayo anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kasmu Majaliwa Majaliwa.