Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Dkt.Selemani Jafo(Mb) amezitaka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki( EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuendeleza teknolijia ya matumizi bora ya nishati


Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt.Selemani Jafo(Mb) amezitaka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki( EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuendeleza teknolijia ya matumizi bora ya nishati

Waziri Jafo ameyasema hayo wakati wa kufunga mkutano wa Kikanda wa Matumizi Bora ya Nishati uliohusisha Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliomalizika leo Desemba 05,2024 jijini Arusha.

Amesema lengo la nchi ni kuendelea kukuza uchumi, viwanda vifanye kazi kwani maendeleo ya Viwanda yanategemea uwepo wa Nishati ya kutosha hasa katika kuinua uchumi na biashara zifanyike kwa ufanisi lakini hilo litawezekana ikiwa kuna nishati ya kutosha ambayo uwepo wake unategemea usahihi katika matumizi yake.

Amesema kuwa Tanzania ina matumizi bora ya nishati ambapo kwa sasa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linaandaa viwango fanisi vya vifaa vya nishati vinavyozalishwa au kuingizwa nchi ambavyo vitawezesha nchi kutumia umeme kwa ufanisi.

Vile vile Dkt.Jafo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tqnzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya Nishati ambapo uwekezaji huo una maana kubwa katika kuendeleza viwanda na biashara

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk,Khatibu Kazungu amesema serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati imejipanga kutekeleza Mkakati wa Matumizi Bora ya Nishati uliozinduliwa tarehe 4 Desemba 2024 kwa kuhakikisha Mkakati huo unatekelezwa kwa kuwekewa bajeti ili nchi iweze kuwa na ufanisi katika vifaa vya nishati.

Amesema kupitia Mkutano wa REEC 2024 maazimio mbalimbali yamefikiwa ikiwemo kufanya tafiti za pamoja ili kuboresha matumizi bora ya nishati na kuihusisha kikamilifu Sekta Binafsi.

Naye , Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso ameipongeza serikali kwa kuendesha na kusimamia mkutano wa REEC 2024 ulioleta mafanikio makubwa ikiwemo mafunzo na kubadilishana uzoefu ili kuwa na ufanisi kwenye matumizi ya nishati.