Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Dkt. Selemani Jafo (Mb) amekutana na Kamati ya tathmini ya biashara baina ya wazawa na wageni pamoja na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo


Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo (Mb) amekutana na Kamati ya tathmini ya biashara baina ya wazawa na wageni pamoja na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo na Wadau mbalimbali wa biashara nchini kwa lengo la kupata mrejesho wa ripoti hiyo iliyowasilishwa hivi karibuni ili kuleta maslahi ya wafanyabiashara wazawa nchini, iliyofanyika Mei 5, 2025 jijini Dar es salaam.

Katika kikao hicho Waziri Jafo amesema kuwa wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani imekubaliana kuweka utaratibu maalum wa vibali kwa wageni wanaoingia nchini kwa ajili ya kufanya biashara.

Amesema kwa mujibu wa taarifa kutoka Idara ya Uhamiaji, jumla ya watu 62 wameondoshwa nchini kwa kosa la kufanya biashara bila kuwa na vibali maalum na zoezi hilo linaendelea hatua kwa hatua kuhakikisha kila kilichoagizwa kinatekelezwa ipasavyo.

Dkt. Jafo amesisitiza kuwa taarifa hiyo iwe kama muongozo na kioo kwa sekta zote kwa lengo la kulinda maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.Suleiman Serera, amesema kuwa utekelezaji wa maagizo ya waziri unaendelea vizuri kupitia kamati ya tathmini ya hali ya biashara kati ya wazawa na wageni katika Soko la Kariakoo

Pamoja na hayo Dkt.Serera amesema baadhi ya taasisi zilizo chini ya wizara hiyo zimeendelea kutekeleza maagizo yaliyotolewa ikiwemo BRELA imekamilisha andiko la marekebisho ya sheria ya makampuni na leseni za biashara, ambalo linaeleza ni biashara zipi zinapaswa kufanywa na wazawa na zipi na wageni na Ukaguzi umeanza kubaini kampuni zinazokiuka masharti ya leseni.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe.Albert Chalamila, amemshukuru Dkt. Jafo kwa juhudi zake kuhusu biashara nchini hasa Kariakoo na kusisitiza kuwa kama suala hilo limepangwa vizuri, hakuna kitakachoshindikana.

Mhe. Chalamila ameeleza kuwa lengo la kuruhusu biashara kufanyika kwa saa 24 lilikuwa ni kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya serikali masaa yote, kwani awali ukusanyaji ulikuwa unaishia saa 12 jioni.