Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Dkt. Serera: Changamkieni Fursa Katika Sekta ya Magari Tanzania


Dkt. Serera: Changamkieni Fursa Katika Sekta ya Magari Tanzania

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera, ametoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya magari nchini, hususan katika uundaji wa magari madogo ya abiria na utengenezaji wa vipuri.

Vilevile, amebainisha kuwa Serikali imedhamiria kuweka mazingira bora na wezeshi yanayolenga kukuza viwanda na uzalishaji ili kukuza maendeleo ya minyororo wa thamani wa usafirishaji wa ndani, kukuza maendeleo ya ujuzi na uhawilishaji wa teknolojia, na kuimarisha miundombinu ya huduma baada ya mauzo.

Dkt. Serera ameyasema hayo Julai 05, 2025 wakati akizindua rasmi Mwezi wa kwanza wa Huduma wa ANDA-SHACMAN nchini Tanzania, ulioandaliwa na ANDA AUTO LIMITED katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam.

Dkt. Serera pia amesisitiza kuwa uundaji wa magari madogo ya abiria na utengenezaji wa vipuri utasaidia kukidhi mahitaji ya usafiri nchini, kuongeza ajira, na kupunguza uagizaji wa magari hayo na vipuri kutoka nje ya nchi.

“Mwezi wa kwanza wa Huduma wa ANDA-SHACMAN ni muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa teknolojia za kisasa za magari na wataalamu wenye ujuzi katika sekta ya usafirishaji nchini,” alisema Dkt. Serera.

Vile vile, amebainisha kuwa huduma za usafirishaji mizigo zina jukumu muhimu katika kukuza uchumi nchini, Japo hadi sasa Tanzania ina viwanda 13 vya kuunganisha magari, nchi hii ina soko kubwa kwa sekta hiyo kwa kuwa kijiografia inapakana na nchi sita zisizo na bandari na kuwa na miundombinu muhimu ya bandari inayoihusisha katikati ya biashara na usafirishaji wa kikanda.

“Tunaamini kabisa kwamba kwa jitihada za ushirikiano, Tanzania inaweza kubadilika kutoka kuwa muagizaji mkuu na kuwa kituo chenye ushindani kwa utengenezaji na usambazaji wa magari katika kanda,” alisema Dkt. Serera.

Aidha, amebainisha kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na wa kimataifa kuboresha mifumo ya udhibiti, kuwekeza katika miundombinu inayounga mkono, na kufungua fursa mpya za ukuaji ndani ya sekta ya magari na kwingineko.