Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Elimu ya Utekelezaji wa MKUMBI Ienee hadi Vijijini


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Erick Shigongo (Mb) ameipongeza Wizara kwa kutekeleza Mpango wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini (MKUMBI) na kutaka kutoa elimu ya utekelezaji huo hadi vijijini ili wananchi waielewe.

Ameyasema hayo wakati wa Kikao cha Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Oktoba 24, 2022 kilichopokea na kujadili taarifa ya Utekelezaji wa MKUMBI ambao umekuwa ukijulikana kama “BLUEPRINT” Bungeni, Dodoma

Akijibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na Wajumbe wa Kamati, Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) amesema kuwa utekelezaji wa MKUMBI unaoendelea umegusa sekta zote na yanalenga kuifiki

ha Nchi yetu kuwa miongoni mwa Nchi ambazo ufanyaji Biashara na uwekezaji unavutia na ni rahisi. Awamu ya Sita imejikita katika kuhakikisha inaweka miundombinu wezeshi kama Umeme, Maji, Barabara, pamoja na mifumo yote ya Kieletroniki ili kurahisisha utoaji huduma kwa Wawekezaji pamoja na kufuta kodi mbalimbali ambazo zilikuwa kero kwa Wawekezaji.

Naye Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bw. Ally Gugu amesema MKUMBI imewezesha wawekezaji katika sekta ya Kilimo, Mifugo na Viwanda ambavyo vimepata fursa ya kuuza nyama iliyochakatwa nje ya Nchi kupitia kiwanda cha Eliya Food na Tanchoice

Awali akiwasilisha taarifa ya MKUMBI Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Kuboresha Mazingira cha Wizara Bw. Baraka Aligaesha amesema kuwa kazi kubwa imefanywa katika sekta zote na imesaidia kufutwa ama kupunguzwa kwa Tozo, Ada na Faini 232 ambazo zilikuwa zikitozwa na Mamlaka mbalimbali za Udhibiti.

 Bw. Aligaesha amesema pia kuwa Sheria na Kanuni 40 zimepitiwa na kufanyiwa marekebisho pamoja na Taasisi zilizokuwa na Muingiliano wa Majukumu zimeunganishwa ili kuboresha mazingira ya biashara nchini.