Habari
Fanyeni kazi kwa ubunifu, weledi, utayari na kwa wakati katika kuwahudumia wawekezaji, wazalishaji na wafanyabiashara

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) amewataka Wakuu wa Idara na Taasisi zilizochini ya Wizara kufanya kazi kwa ubunifu, weledi, utayari na kwa wakati katika kuwahudumia wawekezaji, wazalishaji na wafanyabiashara ili kukuza uchumi na kutumiza malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Waziri Kijaji ameyasema hayo alipokuwa akiongea katika kikao na Wakuu wa Idara na Taasisi zilizochini ya Wizara kilichofanyika Mei 18 2022 jijini Dodoma. Kikao hicho kililenga kupokea na kujadili mipango kazi ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara iliyopitishwa Mei 9, 2022.
Waziri Kijaji akiwa ameambatana na Viongozi wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara wakiwemo Naibu Waziri Mhe. Exaud Kigahe (Mb.) Katibu Mkuu Prof. Godius Kahyarara na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Hashil Abdallah aliwata Wakuu wa Idara na Taasisi hao pia kutatua kero mbalimbali za wawekezaji, wazalishaji na wafanyabiasharai ili kuwawezesha wafanye shughuli zao kwa ufanisi na kuendeleza sekta ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.
Nao Wakuu wa Idara na Taasisi hizo zikiwemo TIC, NDC, EPZA, TIRDO, TEMDO, CAMARTEC, SIDO, NEEC, TBS, WMA, TANTRADE, BRELA, FCC, FCT, CBE na WRRB walipokea maelekezo yaliyotolewa na kuahidi kuyatekeleza ndani ya kipindi kilichopangwa ili kukuza biashara, kuvutia uwekezaji na hatimaye kuongeza pato la Taifa, Ajira na kukuza uchumi.