Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI YADHAMIRIA KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI YA BIASHARA NA USHINDANI WA HAKI KUPITIA AKILI MNEMBA


Serikali imesema kuwa itahakikisha wafanyabiashara wanapata mazingira wezeshi ya biashara, kupata faida na kuchangia katika ukuaji endelevu wa uchumi wa Taifa.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Patrobas Katambi (Mb), alipomuwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb) katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ushindani Duniani, yaliyofanyika Disemba 05, 2025 jijini Dar es Salaam.

Kauli mbiu ya mwaka huu, “Akili Mnemba (AI) katika Kudumisha Ushindani wa Haki na Kulinda Walaji”, inalingana na dhana ya kimataifa ya Artificial Intelligence (AI), Consumers and Competition Policy, ikisisitiza kuwa teknolojia ya AI ni zana muhimu katika kudumisha ushindani wa haki, kulinda maslahi ya walaji na kuongeza uwazi katika masoko.

“Serikali imejipanga kuwa daraja, si ukuta kuhakikisha sera zinazolinda walaji na wafanyabiashara zinatekelezwa ipasavyo, hususan katika matumizi ya TEHAMA na AI,” alisema Mhe. Katambi, akiweka mkazo katika uwekaji wa mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na walaji.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Hadija Ngasongwa amesema maadhimisho yalianza kwa shughuli za kijamii, ikiwemo utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu haki zao, umuhimu wa uwazi katika masoko na namna ya kuepuka vitendo vinavyokandamiza ushindani.

Pia Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani (FCT), Jaji Rose Ebrahim, amewashauri wananchi na wafanyabiashara kutoa taarifa za vitendo viovu visivyo vya haki katika soko, huku Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani, Dkt. Aggrey Mlimuka, akisisitiza uhusiano kati ya AI na ulinzi wa walaji, akibainisha kuwa teknolojia inasaidia kuhakikisha uwazi na ufanisi katika Biashara.