Habari
SERIKALI YADHAMIRIA KUMALIZA MGOGORO WA MAFAO YA WAFANYAKAZI 760 SPM MGOLOLO
Serikali imesema ina nia ya kuhitimisha mgogoro uliopo baina yake na wafanyakazi wapatao 760 wa kiwanda cha karatasi cha Southern Paper Mills Ltd (SPM Mgololo), ambao wanadai mafao ya utumishi wao yaliyopaswa kulipwa kabla ya kubinafsishwa kwa kiwanda hicho, ili kuhakikisha wananchi hao wanapata haki zao stahiki.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dennis Londo (Mb), Bungeni jijini Dodoma Aprili 8, 2026 akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mafinga Mjini Mhe. Dickson Lutevele aliyetaka kujua ni lini Serikali itakamilisha malipo ya mafao kwa wafanyakazi 760 wa kiwanda cha SPM Mgololo walioshinda kesi tangu mwaka 2007, ili kuonyesha nia yake ya dhati ya kumaliza mgogoro huo na kuwapatia wananchi hao haki yao.
Mhe. Londo amefafanua kuwa Serikali inahusika katika suala hilo kama mmiliki wa awali wa kiwanda hicho kabla ya kubinafsishwa, na kubainisha kuwa mwekezaji ameshalipa sehemu ya madai yaliyokuwa yanamhusu.
Awali akijibu swali la Msingi namba 35 ambalo Mhe. Dickson Lutevele aliuliza ni lini malipo ya madai ya waliokuwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Karatasi (SPM Mgololo) yatafanyika? Mhe. Londo ameeleza kuwa kiwanda cha SPM kilibinafsishwa Februari 2004 kwa kampuni ya RAI Group. Kufuatia hatua hiyo, takriban wafanyakazi 760 walifungua shauri namba 162/2017 katika Mahakama ya Kazi dhidi ya Serikali wakidai mafao yao ya kabla ya ubinafsishaji, suala ambalo hadi sasa bado lipo mahakamani.
