Habari
SERIKALI YAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUWEKEZA KIWANDA CHA KUKOBOA KAHAWA
Wizara ya Viwanda na Biashara imewaita wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika kiwanda cha kukoboa kahawa kilichopo Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma ili kuleta manufaa kwa wakulima.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), Februari 2, 2026 Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Nyasa, John Nchimbi.
Katika swali lake, Mbunge huyo ametaka kufahamu mpango wa Serikali wa kujenga kiwanda cha kukoboa kahawa cha Nyasa, kama ilivyoahidiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Londo amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa huzalisha kahawa aina ya Arabica kwa wastani wa tani 2,193.3 kwa mwaka.
Ameeleza kuwa Serikali, kupitia Halmashauri ya Nyasa, imetenga eneo lililopo Kitongoji cha Ndanda, Kijiji cha Kingiritiki, Kata ya Kingiritiki, kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho.
Kwa mujibu wa Londo, eneo hilo lina ukubwa wa hekta nne (sawa na eka 10) na lina miundombinu wezeshi ikiwemo barabara, maji na umeme.
Katika swali la nyongeza, Mbunge Nchimbi amehoji kwa nini Serikali isianze moja kwa moja utekelezaji wa mradi huo badala ya kusubiri wawekezaji kutoka sekta binafsi, hali inayochukua muda mrefu.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri Londo amesema utekelezaji tayari umeanza, ambapo miche ya kahawa milioni mbili imetolewa kwa wakulima, hatua iliyoongeza uzalishaji wa zao hilo.
