Habari
SERIKALI KUJENGA KIWANDA CHA SARUJI HANANG
Serikali imesema inatafuta Mwekezaji wa uhakika kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda cha kuzalisha Saruji Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara, kwa kuwa kuna malighafi za kutengeneza Saruji.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb) Mei 11, 2026 Bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akijibu Swali namba 305 la Mbunge wa Hanang Mhe. Asia Halamga, aliyetaka kujua Mpango wa Serikali wa kuanzisha Kiwanda hicho kutokana na uwepo wa malighafi za kutosha Wilayani humo.
Akijibu Swali hilo, Naibu Waziri Londo amesema Serikali inatambua uwepo wa malighafi zinazotumika kuzalisha Saruji katika Wilaya ya Hanang’ na tayari imeweka mazingira ya utekelezaji wa mradi huo.
Amesema Serikali imetenga eneo la ekari 360 kwa ajili ya mradi huo, ambapo ekari 300 ni eneo lenye malighafi huku ekari 60 zikitengwa kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda huku hatua za kutafuta Mwekezaji zikiendelea ili kuhakikisha ujenzi wa Kiwanda hicho unaanza na kusaidia kukuza uchumi wa eneo hilo pamoja na kuongeza ajira kwa Wananchi.
Londo amefafanua kuwa mkakati huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayosisitiza ujenzi wa Viwanda vya kimkakati kulingana na rasilimali zilizopo katika kila Mkoa. Amebainisha kuwa mbali na Saruji, Hanang’ ina utajiri wa malighafi za uzalishaji wa Chumvi pamoja na fursa kubwa katika zao la Ngano, maeneo ambayo Serikali inayaandaa kwa ajili ya uwekezaji wa kuongeza thamani ili kuimarisha soko la ndani na nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, ameeleza kuwa mpango wa kuimarisha Viwanda hautaishia Hanang pekee, bali unahusisha pia Wilaya ya Babati na maeneo mengine nchini kupitia uanzishwaji wa kanda maalum za uwekezaji kwa lengo la kuongeza thamani, kukuza mauzo ya nje, na kupaisha uchumi wa Wananchi kulingana na vipaumbele vya Kitaifa.
