Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI KUIMARISHA SEKTA YA VIWANDA KUKUZA UCHUMI WA TAIFA


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuimarisha sekta ya viwanda kama muhimili mkuu wa mageuzi ya kiuchumi, uzalishaji wa ajira, na maendeleo endelevu nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dennis Londo (Mb), katika hafla ya Iftar na majadiliano ya viongozi wa viwanda iliyodhaminiwa na kampuni ya Africab Group jijini Dar es Salaam Machi 17, 2026 ambapo amesisitiza kuwa lengo ni kuongeza thamani ya rasilimali za nchi, kupanua uwezo wa uzalishaji bidhaa, na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Amesisitiza umuhimu wa sekta binafsi hususan viwanda vinavyowakilishwa na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) kuwa na mchango mkubwa kupitia uwekezaji, ubunifu, na uthubutu unaochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kiteknolojia na kuahidi kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji wa viwanda nchini.

Naibu Waziri Londo, amebainisha kuwa ushirikiano baina ya sekta binafsi na Serikali ni muhimu katika kutatua changamoto za miundombinu, nishati, na mifumo ya kisheria.

Amesema Serikali inachukua changamoto zilizobakia na kwenda kuzifanyia Kazi ili kuimarisha mazingira ya Uwekezaji kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza shughuli za mnyororo wa biashara nchini.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Mhe. Laurent Luswetula (Mb), amesema Wamepokea changamoto ambazo Wamiliki wa Viwanda wameziwasilisha ambapo nyingi zinahusu masuala ya kodi kodi za bidhaa na kuahidi kwamba zitatatuliwa Kwa maamuzi ya pamoja baina ya Wizara hiyo na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI).

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CTI Mhandisi Leodegar Tenga amesema katika hafla hiyo wamezungumza mambo ambayo yatasaidia sekta ya viwanda kufanya vizuri jambo litakalochochoea ukuaji wa uchumi na ajira katika dunia ya ushindani.