Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI YAMTAKA MWEKEZAJI KUTOKA BURUNDI KUHARAKISHA MRADI WA KIWANDA CHA SARUJI KASULU


Mwekezaji wa Kampuni ya TACECO Ltd kutoka Burundi kuharakisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha Saruji Kasulu, mradi ambao ni muhimu kwa wananchi wa eneo hilo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), Februari 4 2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kasulu Vijijini, Mhe. Edibily Kinyoma.

Katika swali lake, Mbunge huyo amehoji ni lini ujenzi wa kiwanda cha Saruji cha Kasulu utaanza ukizingatia mwekezaji alishapewa eneo miaka mitatu iliyopita.

Akijibu swali hilo, Londo amekiri kuwa ni kweli eneo lililopo katika kata ya Kagera Nkanda katika Wilaya ya Kasulu lilitolewa kwa mwekezaji wa Kampuni ya TACECO Ltd kutoka Burundi kujenga kiwanda cha saruji.

Amesema hata hivyo kasi yake imekuwa ndogo katika kutekeleza mradi huo, na kwa sasa Serikali inaendelea kumhimiza kuhakikisha mradi huo unaanza utekelezaji haraka iwezekanavyo.

Katika swali la nyongeza, Mbunge huyo amehoji Serikali haioni haja ya kurudisha eneo hili kwa wananchi kwasababu kwa sasa linatumika kwa kazi nyingine ya kilimo cha maharage na mahindi.

Akijibu swali hilo, Londo amesema watamwita mwekezaji wafanye nae mazungumzo ili eneo litumike kwa kazi iliyokusudiwa na si vinginevyo.