Habari
SERIKALI YAWATAKA WANAWAKE KUTUMIA VIWANGO VYA UBORA VYA TBS
Serikali imetoa wito kwa Wanawake Wajasiliamali nchini kuacha kuogopa taratibu za udhibitishaji wa ubora, badala yake watumie viwango vya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kama daraja la kufikia masoko makubwa ya ndani na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa Machi 14, 2026, na Dkt. Ashura Katunzi, aliyemwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), katika kilele cha Mkutano wa Wanawake Viongozi na wafanyabiashara (Accelerate Women’s Executive Summit) uliofanyika katika hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika Mkutano huo kwa niaba ya Waziri, Dkt. Ashura Katunzi amesisitiza kuwa viwango vya ubora si vikwazo vya biashara, bali ni nyenzo muhimu zinazohakikisha usalama, uaminifu, na ushindani wa bidhaa sokoni.
Aidha, amewahimiza Wanawake Wajasiliamali kuanzia wale wanaofanya shughuli zao majumbani, mashambani, au katika karakana ndogo kufuata miongozo ya TBS ili kugeuza mawazo yao kuwa biashara endelevu zinazoweza kuingia kwenye maduka makubwa (supermarkets) na hata kusafirisha bidhaa nje ya mipaka ya Tanzania.
Dkt. Katunzi pia amebainisha kuwa Serikali, kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, inaendelea kupanua mipango inayosaidia ujasiriamali, uanzishaji wa viwanda, na kurahisisha upatikanaji wa masoko kwa biashara ndogo na za kati (SMEs) zinazoongozwa na Wanawake.
Amesema kuwa mafanikio katika soko la kisasa yanahitaji zaidi ya juhudi tu; yanahitaji ubora usioyumba na uaminifu kwa walaji, jambo ambalo linawezekana kupitia udhibitishaji na vipimo rasmi vya mamlaka husika.
Dkt. Katunzi amesema kuwa kila biashara inayostawi inayoongozwa na mwanamke inatengeneza ajira, inaimarisha jamii, na inatoa hamasa kwa kizazi kijacho cha wasichana kuona kuwa inawezekana kufika kileleni mwa uongozi na biashara.
Vilevile , amewahimiza Wanawake hao washiriki wa mkutano huo kushirikiana na kubadilishana maarifa ili kutengeneza fursa zaidi kwa wanawake wengine kuinuka.
Dkt Katunzi pia , amewafafanulia na Kuwaitis Wanawake hao kuwa mwanamke anapofanikiwa, familia inastawi na Taifa zima linapiga hatua kuelekea maendeleo ya kiuchumi
