Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Home WAZIRI KIJAJI AWATAKA WATANZANIA KUWAPOKEA WAWEKEZAJI


Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji ameshuhudia utiaji saini wa Mkataba wa Makabidhiano  kati ya  Kampuni ya Elsewedy Industrial Development  na Property International unaohusu  ardhi  ya eneo litakalotumika katika mradi wa ujenzi wa  kongani ya viwanda ( Industrial Park) itakayochangia kuimarisha uchumi wa nchi.

Akiongea katika makabidhiano hayo yaliyofanyika  Machi 9, 2022 Dkt. Kijaji amesema  makabidhiano hayo ni hatua kubwa ya  utekelezaji  wa mradi wa kimkakati uliopo Kisarawe II Kigamboni unaohusisha  ujenzi wa kongani ya viwanda yenye eneo la ukubwa wa mita za mraba milioni 2.2 ambayo ni kubwa kwa Afrika Mashariki.

Dkt. Kijaji pia amesema utekelezaji wa Mradi huo unaojumuisha ujenzi wa kongani ya viwanda vikiwemo viwanda vya kutengeneza nguo, madawa na uunganishaji magari  unaotarajia kuzalisha ajira  takribani 50, 000 za moja kwa moja  ni utekelezaji wa malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kulifungua  Taifa kiuchumi.

Aidha, Dkt. KIjaji  ametoa wito kwa Watanzania kuwa tayari kwa kuwapokea wawekezaji na kutoa bei nzuri ya ardhi yenye faida kwa pande zote mbili pamoja na kutumia fursa zitakazojitokeza kutokana na  mradi huo kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kushirikiana na wawekezaji hao ili kukuza ajira na uchumi katika nchi yetu.

Vile vile, Dkt. Kijaji ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza Tanzania kwa kuwa Tanzania ni salama, iko tayari na inaendelea kuweka mazingira bora ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama barabara, umeme na maji kwa wawekezaji na wafanyabiashara.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof  Godius Kahyarara amesema  kazi ya ujenzi wa mradi huo unaojumuisha viwanda 100 katika kongani hiyo umeanza na utaiweka Tanzania katika Ramani ya Vinara wa Uchumi shindani kwa Afrika.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Dkt. Maduhu Kazi amesema TIC itaendelea kutoa msaada na ushirikiano kwa mwekezaji huuo katika kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa haraka na kwa ufanisi.