Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SEKTA YA VIWANDA NA BIASHARA YATAJWA KAMA MUHIMILI MKUU WA UCHUMI WA TAIFA


Sekta ya viwanda na biashara ni mhimili muhimu katika safari yamaendeleo ya Taifa kwa kuongeza thamani ya malighafi, mapato ya Taifa, kuingiza fedha za kigeni, na kuchochea ubunifu wa teknolojia na kutoa ajira.

Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali ya Awamu ya Sita imejikita katika kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuchochea ubunifu wa teknolojia na kujenga uchumi shindani, jumuishi, na endelevu unaoendana na maono ya Dira ya Taifa ya mwaka 2050.

Hayo yamesemwa na Makamu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Profesa Emmanuel Munishi, kwa niaba ya Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Denis Londo, Machi 27, 2026 wakati akizindua Taarifa ya Utafiti wa Ukaguzi wa Uhuru wa Kiuchumi Tanzania 2024 wakati wa
Mkutano wa Kilele cha Wiki ya Uhuru wa Kiuchumi (Uhuru Economic Week 2026 uliofanyika jijini Dar es Salaam,

Aidha, Profesa Munishi amebainisha kuwa Taarifa hiyo ya Uhuru wa Kiuchumi inatoa mchango mkubwa katika kuibua hoja za kisera na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mazingira ya biashara.

Amesema kuwa kupitia tafiti hizo, Serikali inapata mwongozo wa kisayansi wa namna ya kuimarisha uhuru wa kiuchumi, ambao uzoefu wa kimataifa unaonyesha kuwa nchi zenye uhuru huo hupata ukuaji wa haraka wa uchumi na ustawi wa wananchi.

Vilevile amebainisha kuwa Kwa mujibu wa tathmini ya kimataifa ya Uhuru wa Kiuchumi ya mwaka 2023, Tanzania ilipata alama ya 6.34 kati ya 10 na Kushoka nafasi ya 8 kati ya Nchi 24 za Afrika Mashariki na Kusini na hivyo kukuza uchumi kwa wastani wa asilimia 5 hadi 6 kwa mwaka

Prof. Munishi pia amebainisha kuwa Mafanikio hayo yamechangiwa na Uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, ambaye kupitia diplomasia ya uchumi na mageuzi ya kisera, ameiwezesha nchi kuvutia uwekezaji wa kigeni (FDI) unaokadiriwa kufikia dola bilioni 1.1 kwa mwaka 2023.