Habari
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeipongeza Serikali

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeipongeza Serikali kwa jitihada zilizofanywa kufanikisha ujenzi na uendelezwaji wa kiwanda cha kuzalisha Viuadudu (Tanzania Biotech Products Ltd - TPBL.
Hayo yamesemwa Machi 17, 2023 katika ziara ya Kamati hiyo kutembelea kiwanda cha kutengeneza dawa ya kuua viluilui vya mazalia ya mbu kilichopo katika kongani ya Viwanda ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) iliyopo kibaha Mkoani Pwani.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. David Kihenzile (Mb) amesema kuwa kiwanda hicho kina umuhimu mkubwa katika kuhakikisha nchi yetu inaondokana na ugonjwa wa Malaria ambao umekuwa ukisababisha vifo vingi hasa vifo vya mama na mtoto hivyo ni wakati sahihi sasa kama nchi kuibeba ajenda ya Malaria kuwa ya kitaifa katika kuutokomeza ugonjwa huo.
Awali akijibu michango ya baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) amesema kuwa kiwanda hiki cha Viua dudu kilianza uzalishaji rasmi mwaka 2017 ambapo uwezo wa uzalishaji wa kiwanda ni lita milioni sita kwa mwaka na kinatumia malighafi inayopatikana ndani ya Nchi kwa asilimia tisini na nane.
Waheshimiwa wajumbe wa kamati wamepata fursa ya kukagua na kuona shughuli za kiwanda kuanzia katika hatua ya awali ya uzalishaji hadi ufungashaji wa dawa hizo.